13 December 2012
Bulembo avihadharisha vyama vya upinzani
Na Mwandishi Wetu, Simiyu
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Bw.
Abdallah Bulembo, amevitaka vyama ya upinzani nchini
vikae chonjo katika Uchaguzi Mkuu na kudai siku zao
zinahesabika.
Alisema katika uchaguzi huo, vyama hivyo visitarajie kupata ushindi mwepesi kama walioupata katika Uchaguzi Mkuu uliyepita kwani CCM Imejipanga vyema kurudisha mitaa, vijiji, kata na majimbo yote yaliyochukuliwa na upinzani.
Bw. Bulembo aliyasema hayo jana mjini Simiyu kwa nyakati tofauti katika mwendelezo wa ziara yake mkoani humo ili kukagua uhai wa chama hicho, jumuiya zake pamoja na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
“Ni ndoto kwa wapinzani katika Uchaguzi Mkuu ujao kupata
ushindi kama wa mwaka 2010, ushindi ule ulikuwa wa rahisi kutokana na tofauti za wana CCM wenyewe zilizojitokeza
wakati wa kura za maoni.
“Baada ya kura za maoni, baadhi ya wana CCM waligawanyika
na kuwa katika makundi, wengine waliamua kukisaliti chama na kuamua kuwasaidia wapinzani lakini hivi sasa tumezika tofauti
zetu na kuwa kitu kimoja tayari kwa kuisambaratisha kambi ya upinzani kwenye uchaguzi ujao,” alisema Bw. Bulembo.
Pamoja na kambi ya upinzani kupewa nafasi ya kushinda, bado walishindwa kuitumia vizuri nafasi hiyo kupeleka maendeleo
kwa wananchi badala yake wanatumia muda mwingi kuzunguka, kupanda katika majukwaa na kuishambulia Serikali ya CCM na kudai katika kipindi chote cha utawala wake haijafanya kitu.
“Mwenye macho haambiwi tazama, pamoja na maendeleo yote yaliyoletwa na Serikali ya CCM katika nyanja mbalimbali wezetu hawayaoni,” alisema Bw. Bulembo na kuwataka wananchi waone umuhimu wa kuwaadhibu wapinzani kwa kuwanyima kura katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mapema akisoma risala kwa Bw. Bulembo, Katibu wa CCM mkoani humo, Bi. Hilda Kapaya, alisema hali ya kisiasa katika Mkoa huo si shwari kutoka na wapinzani kujitwalia baadhi ya majimbo na kata.
Alisema Mkoa huo una majimbo saba ambapo CCM ilishinda majimbo matatu ambayo ni Busega, Kisesa na Bariadi Magharibi ambapo majimbo ya Maswa Magharibi, Maswa Mashariki na
Meatu yamechukuliwa na CHADEMA wakati Jimbo la Bariadi Mashariki, lipo mikononi mwa chama cha UDP.
Akizungumzia uchaguzi wa madiwani, Bi. Kapaya alisema CCM imeshinda viti 78 wakati upinzani imejinyakulia viti 33 ambavyo vimekwenda katika vyama vya CHADEMA, UDP na CUF.
Hata hivyo, Bi. Kapaya alimuhakikishia Bw. Bulembo kuwa Mkoa huo umejipanga kuipigania CCM ili iweze kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment