03 December 2012

OUT yafanya tathmini ubora wa elimu


Na Mariam Mziwanda

UONGOZI wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) umefanya tathimini ya ubora wa elimu itolewayo chuoni hapo pamoja na kuzingatia taratibu za kufanyatafiti kwa wanafunzi hasa wa sheria ili kuzidi kukipa uwezo chuo hicho.


Akizungumza Jijini Dar es Salaam juzi katika warsha ya kujitathimini kiutendaji iliyowashirikisha wafanyakazi, wakufunzi wa chuo hicho na wadau wa elimu nchini Mkurugenzi wa udhibiti wa ubora chuoni hapo Dkt. Paul Kihwelo alisema imefika wakati sasa OUT kujiimarisha katika utoaji elimu bora.

Dkt.Kihwelo alieleza kuwa mikakati ya OUT ni pamoja na kuangalia kwa undani ubora wa elimu waitoayo, machapisho na tafiti ili kila anayesoma chuoni hapo aendelee kuwa mwanga katika jamii.

Alisema mbali ya chuo hicho kukabiliwa na changamoto za fedha majengo na vitendea kazi lakini wanahakikisha wasomi wake wanapata elimu na nidhamu kuwa kipaumbele cha chuo.

Pia alieleza mafanikio waliyoyapata kutokana na tathimin ya awali iliyofanywa na kamati ya vyuo vikuu ambayo ilionyesha ubora wa chuo hicho na kupewa tena ithbati kwa miaka mitano ijayo.

"Ni faraja ya Watanzania kwa ujumla kwa OUT kuonekana na kamati ya vyuo vikuu katika ubora wa elimu na hatimaye kupewa ithbati kwa miaka mitano tena lakini bado changamoto tulilizopewa na kamati hiyo tutazifanyia kazi ili kufikia malengo zaidi,"alisema.

Alisema ana imani kitengo cha sheria na masomo yake yana muongozo hivyo ni vyema ikazingatiwa kwa maslahi ya jamii nzima.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof.Tolly Mbwete alisema warsha hiyo ambayo ni fursa ya mara mbili kwa mwaka imesaidia kubaini changamoto zinazokikabili chuo hicho.

"Kwa mwaka huu tumetumia fursa hii kuangalia ubora wa elimu,miundombinu ya chuo na majengo ambapo kupitia tathimini hizo itasaidia kubaini changamoto zinazokikabili chuo,"alisema.

Pia alisema lengo la tathimini ya uwezo wa chuo na tafiti mbalimbali wanazozifanya ni kuweza kupata wataalamu wenye elimu bora na si bora elimu .

Prof. Mbwete Alisema chuo hicho kimejipanga kufanya vyanzo vyake vya mapato visaidie pia walimu wanaofundisha chuo hicho kutokana na kujiendesha chenyewe kwa miradi inayoibuliwa na wakufunzi na wanachuoni hao.

Pamoja na hali hiyo alieleza mafanikio ya chuo ni kuona wananchi wa ndani na nje wanakubaliana na uwezo wa elimu itolewayo hali ambayo imeungwa mkono kwa kujitokeza kwa wanafunzi wengi kujiunga  na chuo hicho kwa mwaka huu ikidhihirisha imani ya uwepo wa elimu bora itolewayo.

No comments:

Post a Comment