10 December 2012

Mnyika kupigania ubunge wake leo *Hoja za Ng'humbi kusikilizwa na Majaji watatu


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Rufaa jijini Dar es Salaam, leo inatarajiwa kuanza kusikiliza rufaa ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambayo ilitupilia mbali kesi ya uchaguzi iliyokuwa ikipinga ubunge wa Bw. John Mnyika wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Rufaa hiyo imefunguliwa Oktoba 25 mwaka huu na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Hawa Ng'humbi dhidi ya Bw. Mnyika.

Jopo la Majaji watatu ndio litasikiliza rufaa hiyo akiwemo
Natharia Kimaro, Salum Massati na Catherine Oriyo.

Bi. Ng'humbi amekata rufaa hiyo kupinga hukumu iliyotolewa Mei 24 mwaka huu na Jaji Upendo Msuya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyompa ushindi Bw. Mnyika.

Katika hukumu yake, Jaji Msuya alisema Mahakama hiyo imetupilia mbali madai yote ya mlalamikaji, Bi. Ngh'umbi kwa sababu ushahidi aliouwasilisha ulijikita katika ushahidi wa kusikia ambao Mahakama kamwe haiwezi kuupokea.

Alisema Mahakama hiyo kwa kauli moja inamtangaza Bw. Mnyika kuwa mbunge halali wa jimbo hilo ambapo taratibu zote za uchaguzi ziliduatwa.


Katika kesi hiyo, Bi. Ng'humbi eliyekuwa akitetewa na wakili Bw. Issa Maige, alikuwa akipinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo yaliyompa ushindi Bw. Mnyika.

Bi. Ng'humbi katika hati yake ya madai namba 107/2010, pamoja na mambo mengine aliiomba Mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi wa jimbo hilo ulikuwa batiri kwa sababu haukuwa huru na haki ambapo taratibu za uchaguzi zilikiukwa.

Alidai Bw. Mnyika aliingiza kompyuta ndogo (Laptop), katika chumba cha kuhesabia kura, kuzitumia kwa kujiongezea kula na kumtolea maneno ya kashfa wakati wa kampeni za uchaguzi kwa kumuita fisadi alipokuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (CWT), Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment