10 December 2012

Kesi ya Mnyika yafutwa rasmi *Afikia makubaliano na Hawa Ng'humbi



Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Rufaa jijini Dar es Salaam, jana imekubali ombi la kuiondoa rufaa ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambayo ilitupilia mbali kesi ya uchaguzi iliyokuwa ikipinga ubunge wa Bw. John Mnyika wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).


Rufaa hiyo imeondolewa baada ya aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Hawa Ng'humbi, kufikia makubaliano ya kuiondoa mahakamani.

Oktoba 25 mwaka huu, Bi. Ng'humbi, alikata rufaa mahakamani hapo kupinga hukumu iliyotolewa awali ambapo kesi hiyo ilikuwa ianze kusikilizwa jana lakini iliondolewa baada ya wawili hao kufukia makubaliano nje ya mahakama.

Mbele ya Jopo la Majaji watatu waliokuwa wakiisikiliza kesi hiyo, wakili Bw. Issa Maige ambaye alimwakilisha Bi. Ng'humbi, alidai  shauri hilo limeletwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa rufaa lakini hawataweza kufanya hivyo.

Majaji hao ni Natharia Kimaro, Salum Massati na Catherine Oriyo ambapo Bw. Maige aliongeza kuwa, siku mbili zilizopita, mkata rufaa Bw. Ng'humbi na mjibu rufaa Bw. Mnyika walifanya makubaliano ya kuiondoa rufaa hiyo bila gharama.

Alisema kutokana na makubaliano hayo, anaomba rufaa hiyo iondolewe chini ya kifungu namba 102 (3), kikisomwa pamoja na kifungu namba nne cha sheria za Mahakama ya Rufaa nchini.

“Waheshimiwa Majaji, shauri hili lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini siku mbili zilizopita, mkata rufaa na mjibu rufaa walifanya makubaliano na kuomba rufaa hii iondolewe mahakamani bila  gharama yoyote,” alisema Bw. Maige.

Baada ya maelezo hayo, Jaji Kimaro alitoa uamuzi wa mahakama hiyo kukubaliana na ombi hilo hivyo rufaa hiyo kuondolewa.

Mei 24 mwaka huu, Jaji Upendo Msuya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu iliyompa ushindi Bw. Mnyika.

Katika hukumu yake, Jaji Msuya alisema Mahakama hiyo imetupilia mbali madai yote ya mlalamikaji Bi. Ngh'umbi kwa sababu ushahidi ambao aliuwakilisha ulijikita katika ushahidi wa kusikia ambao mahakama kamwe haiwezi kuupokea.

Alisema Mahakama hiyo kwa kauli moja inamtangaza Bw. Mnyika kuwa mbunge halali wa Jimbo la Ubungo na kwamba taratibu zote za uchaguzi zilifuatwa.

Katika kesi hiyo, Bi. Ng'humbi alikuwa akipinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo yaliyompa ushindi Bw. Mnyika.

Bi. Ng'humbi katika hati yake ya madai namba 107/2010, pamoja na mambo mengine aliiomba mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi wa jimbo hilo ulikuwa batiri kwa sababu haukuwa huru na haki ambapo taratibu za uchaguzi zilikiukwa.

Alidai Bw. Mnyika aliingiza kompyuta ndogo (Laptop), kwenye chumba cha kuhesabia kura, kuzitumia kwa kujiongezea kura na kumtolea maneno ya kashfa wakati wa kampeni za uchaguzi kwa kumuita fisadi alipokuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (CWT) Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Nje ya Mahakama

Bw. Maige alisema, mteja wake amefikia uamuzi huo baada ya kuona muda wa kuendelea na shauri hilo umeenda sana.

Akizungumza na wafuasi wa CHADEMA, Bw. Mnyika  alisema siku chache zilizopita, wakili wa Bw. Maige ambaye ni wakili wa Bi. Ng'humbi, aliwasiliana na wakili wake Bw. Edson Mbogogo ili wafanye makubaliano ya kuiondoa rufaa hiyo mahakamani pamoja na gharama zake.

Alisema alishauriana na wakili wake na kuona ni jambo jema kusamehe hivyo masuala ya kupinga ubunge wake yameisha.

“Ushindi wetu ulikuwa halali, kesi imechukua muda mrefu tangu 2010 hivyo nilikuwa nawatumikia huku nikiendelea na shauri hili, nawashukuru sana kwa ushirikiano wenu,” alisema Bw. Mnyika.

Hata hivyo Bw. Mnyika aliongeza kuwa, pamoja na kuondolewa rufaa hiyo, gharama zake hazitaihusu kesi ya msingi iliyoamuliwa Mahakama Kuu.

Alisema gharama za kesi hiyo zipo palepale hivyo Bi. Ng'humbi anapaswa kuzilipa ingawa hajajua ni kiasi gani atakachomlipa kwani bado hajakaa na wakili wake kufanya mahesabu.

Katika hatua nyingine, aliwataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi katika mikutano yake anayotarajia kuifanya mwisho wa
wiki hii eneo la Manzese na Kata ya Ubungo.

Aliongeza kuwa, katika mikutano hiyo atazungumzia jinsi vigogo wa CCM walivyochagia kuua viwanda kikiwemo cha Urafiki na kusababisha vijana kukosa ajira pamoja na ufisadi uliopo katika Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Baada ya maelezo hayo, wafuasi hao waliondoka eneo la mahakama huku wakishangili na kusema “Hatukubali hadi kieleweke”.

No comments:

Post a Comment