10 December 2012

Mkurugenzi azomewa mbele ya Waziri



Na Yusuph Mussa, Korogwe

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Lewis Kalinjuna na Ofisa Elimu wa halmashauri hiyo, Bi. Mwajabu Kanyemka, jana walizomewa na walimu mbele ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philipo Mulugo.

Walimu hao walichukua uamuzi huo baaada ya Bw. Mulugo kufanya ziara ya ghafla wilayani Korogwe na kupata fursa ya kuzungumza na walimu katika ukumbi wa halmashauri hiyo
ili kusikiliza kero mbalimbali walizonazo.

Kabla walimu hao hawajaanza kutoa kero zao, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo, aliwachongea watendaji wa halmashauri hasa Idara ya Elimu na kudai haiwatendei haki walimu kwa kuwapa siku moja katika wiki ili kwenda kueleza shida zao.

“Mheshimiwa Naibu Waziri, kabla haujaja mimi nimetembelea baadhi ya shule na kupata kero za walimu, kwanza wanadai siku moja waliyopewa ili kutoa kero zao haitoshi, nilimwandikia Mkurugenzi barua lakini hakuna mafanikio, lazima tumjue
aliyeshindwa kufuata maagizo.

“Kitambulisho ni haki ya mtumishi lakini walimu wanatakiwa kulipa sh. 2,000 katika halmashauri ili watengenezewe, masjala kwenye halmashauri inalalamikiwa kwa kushindwa kuwahudumia walimu ambao hata wakiomba likizo wanasumbuliwa na kuambiwa wapeleke viambatanisho wakati walipokuwa wakiajiriwa
walipeleka kila kitu,” alisema Bw. Gambo.

Aliongeza kuwa, usumbufu na kero wanazopata walimu zinachangia waichukie Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kudai kama kuna mtu hataki kazi serikalini aende kuwa mjasiriamali.

Kutokana na maelezo hayo, Bw. Mulugo aliwaweka 'kitimoto', watendaji hao ambapo Bw. Kalinjuna alidai walimu wamewekewa siku moja kwa sababu wanakwenda katika ofisi hizo mara kwa mara ambapo Bi. Kanyemka akidai mpango huo umesaidia shule nyingi kufanya vizuri kitaaluma.

Majibu hayo yaliwafanya watendaji hao kuzomewa na walimu ambapo Bw. Mulugo aliwaambia kuwa, hawawezi kuwapangia watumishi siku za kusikilizwa kero zao na utarartibu huo sio
sera ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Bi. Kanyemka alijaribu kutupa mpira kwa wanasiasa na kudai madiwani waliidhinisha siku moja iwe inatumiwa na walimu
kufika katika ofisi za halmashauri.

Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Diwani wa Kata ya Mgombezi, Bw. Omar Chafesi, wote walimkana Bi. Kanyemka na kudai wao walilipinga jambo hilo.

Katika hatua nyingine Bw. Mulugo amemvua cheo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Antakae, Bw. Rashid Shekighenda baada ya wanafunzi 10 wa shule yake kudanganya mitihani ya darasa la saba mwaka 2011 na kumuagiza Bi. Kanyemka amuandikie barua ya kumvua cheo hicho Desemba 10 mwaka huu.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Old Korogwe, Bi. Aloycia Kessy, alisema anapoomba fedha za likizo kwenda kwa mumewe katika Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera, anapewa nauli ya kwenda Moshi alipozaliwa na kudai huo ni ukiritimba ndani ya idara hiyo.

Mwalimu mwingine Bw. Deus Mnkande, alidai sababu kubwa inayowafanya waende kila siku katika Ofisi za halmashauri ni kutokana na watendaji kushindwa kumaliza kero zao na
kuiomba Serikali ione umuhimu wa kuchukua hatua.

Idara hiyo imeweka siku moja ya walimu kusikilizwa matatizo yao katika wiki ambapo walimu wa  shule ya msingi wanasikilizwa kila Jumatano na wale wa sekondari Alhamisi.

2 comments:

  1. HATUPINGI KAULI YA VIJANA WENGI KUPEWA MADARAKA WENGI WA VIJANA WAKO BUNGENI ILA KWA MARA YA KWANZA NIMESHUHUDIA WABUNGE WAKIZOZANA WENYEWE KWA WENYEWE WAKIZOZANA WABUNGE WA CHAMA TAWALA NA SERIKALI YAO KWA MADAI NI KUKUWA KWA DEMOKRASIA MIMI NINA MTAZAMO TOFAUTI KABISA NAONANI MAKOVU YA UTANDAWAZI ULIOANZA KAMA MIAKA 30 ILIYOPITA UKAWAKUMBA VIJANA AMBAO WALIKUWA NA UPEO MDOGO WA KUCHUJA MABAYA YA UTANDAWAZI REJEA MADA"UTANDAWAZI NA MALEZI- [WAJENZI WA DUNIA] NA MDEE MWANAHIZA ;AMESHAURI WAKALA WA MALEZI YA VIJANA WACHUKUE NAFASI ZAO KUWAREKEBISHA VIJANA KWANI UZEMBE WAO UMESABABISHA; vijana kutothaminiana wenyewe kwa wenyewe ;wamekosa umoja na mshikamano kama ndugu wa jamii moja;kuzusha vita vya wenyewe ndani ya jmii moja; umimi,udini,ukabila,ukanda;kukosa mafunzo yoyote ya kimaadili kwa wakubbwa au wadogo zao;wametawaliwa na jazba,hasira,chuki,majivuno,kutunishiana misuli na mizozo isiyo na tija,fujo subira imepotea kabisa.Umaarufundio ngao ya maisha yao ,kudai haki bila kufanya kazi,wkwa kwa kiasi kikubwa na tamaduni za magharibi hivyo kujishugulisha na mambo ya kuiga na kushindwa kufanya mambo ya ubunifu [KUKOSA RASILIMALIWATU] WAKALA WA MALEZI WANASHTUTUMIWA NI 01;FAMILIA 02;TAASISI ZA ELIMU 03;TAASISI ZA DINI 04;MAKUNDI RIKA ;05;VYOMBO VYA HABARI 06;SERIKALI : NI VEMA SERIKALI IRUDISHE MARA MOJA JESHI LA KUJENGA TAIFA SINA UHAKIKA IWAPO LILE LA KUJENGA UCHUMI ZANZIBAR LINA MAUDHUI SAWA VIJANA WA LEO NI YATIMA WA MALEZI YA KITANZANIA

    ReplyDelete
  2. Poleni sana. Sasa uongozi ni kazi. Neno kero lisipopata tafsiri sahihi tutafika wapi?kero mbona ni za kila siku?

    ReplyDelete