10 December 2012

Lipumba aishukia Takukuru



Na Darlin Said

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameituhumu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa kushindwa kuwakamata, kuwachukulia hatua wahusika wa vitendo vya rushwa.

Prof. Lipumba aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mdahalo ulioandaliwa na taasisi hiyo katika kuadhimisha siku ya kupambana na rushwa nchini ili kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali.

Alisema katika chaguzi zilizofanyika hivi karibuni ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), suala la rushwa lilijitokeza kwa
kiasi kikubwa na kusababisha Waziri Mkuu Mstaafu Bw. Fredrick Sumaye rushwa hizo zilitolewa kwa njia ya mtandao.

“Hadi leo, TAKUKURU hatujawasikia wakichukua hatua yeyote ya kukabiliana na tatizo hili hivyo ni vyema wakamuita Bw. Sumaye ili aweze kuwafafanulia zaidi,” alisema Prof. Lipumba.

Aliongeza kuwa, asilimia 70 ya viongozi waliochaguliwa katika chaguzi hizo walitokana na rushwa kwani chama hicho kilipaswa kuwa mfano bora wa kupambana na vitendo hivyo.

“Ingawa wamejitahidi kuvua gamba, hivi sasa limekwama kiunoni hivyo lazima TAKUKURU muwe makini, ili tuweze kutokomeza rushwa, maadili katika uongozi ni suala la msingi hivyo ni muhimu wawe mfano wa kutotoa na kupokea rushwa,” alisema.


Alisema vitendo vya rushwa vinasababisha vijana wengi wawe na imani potofu kuwa ili uweze kufanikiwa lazima uwe na mtu hivyo hali hiyo inachangia wanafunzi kutotilia mkazo elimu wakiamini yupo mtu wa kumsaidia.

“Unapofika wakati wa viongozi kutangaza mali zao, wengi hawasemi ukweli hivyo TAKUKURU mnapaswa kutafakari
kwa makini kwanini wanapata hofu za kuzitangaza.

“Naiomba Serikali ishirikiane na taasisi binasfi ili kutokomeza vitendo hivi ambavyo vinalitia aibu Taifa,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, aliwataka watumishi wa umma kuyatumia maadhimisho hayo kwa kutafakari mchango wao wa kujenga Taifa bora, kuzingatia maadili pamoja na kukabiliana na rushwa.

“Umefika wakati wa kupitia mwongozo wa Taifa wa utawala bora
ili kuboresha na kuweka mambo ambayo yataongeza kasi na ufanisi katika sekta umma, wekeni wazi vikwazo vyote vinavyokwamisha mapambano dhidi ya rushwa,” alisema.

Alisema madili ni silaha kuu ya kukabiliana na vitendo vya rushwa hivyo kila mmoja anatakiwa kutafakari kwa undani mwenendo wake wa kimaisha, kujiuliza na kujijibu kama anazingatia maadili husika.

No comments:

Post a Comment