04 December 2012

Mkanganyiko wa lugha kikwazo cha maendeleo ya elimu nchini



IPO mitazamo tofauti juu ya lugha inayofaa kufundishia kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuoni ili wanafunzi waweze kusoma bila usumbufu.


Kundi moja linasema lugha inayofaa ni Kiswahili na jingine linasema Kiingereza ndio kipewe nafasi.

Kiswahili ndio lugha inayotumika nchini katika shule za msingi ambapo Kiingereza hutumika kama somo linalojitegemea kwa wanafunzi wa darasa la tatu hadi la saba.

Hali hiyo inaleta mkanganyiko miongoni mwa wanafunzi. Zipo badhi ya shule za msingi ambazo hutumia Kiingereza kufundishia masomo mbalimbali na kutumia Kiswahili kama somo la ziada.

Katika shule za sekondari, Kiswahili hutumika kama somo na Kiingereza hutumika kama lugha ya kufundishia jambo ambalo baadhi ya wanafunzi hukosa uelewa mzuri wa masomo ambayo wanafundishwa kutokana na msingi wa lugha ya Kiswahili
ambao wameuzoea toka shule ya msingi.

Kwa kawaida mwanafunzi hupata uelewa zaidi katika lugha anayoweza kuitumia lakini mazingira ya nchi yetu yanachangia kuwafanya wanafunzi wengi kushindwa kuwa wabunifu kupitia elimu wanayoipata kutokana na mkanganyiko huo.


Mwanafunzi unapomtoa katika mazingira ya lugha aliyoizoea na kupata nayo uzoefu wa kuitumia, husababisha akariri masomo badala ya kuelewa na kuwa mbunifu.

Sisi tunasema kuwa, jamii kubwa ya Watanzania ukiondoa wale waishio mijini, wanapozaliwa hujifunza na kuongea lugha zao za asili na wanapoanza darasa la kwanza, hujifunza Kiswahili hivyo mazingira ya kuwahamisha waachane na lugha hiyo ili watumie Kiingereza, inawafanya wakariri masomo yao na kukosa uelewa.

Ni wazi kuwa, Watanzania wengi huzungumza Kiswahili hivyo watoto wanapozaliwa hujikuta wakizungumza lugha hiyo na wanapokwenda shule za msingi, pia hutumia Kiswahili na kuwafanya wawe na uwezo mkubwa wa kuitumia.

Kitendo cha kuwahamisha na kuwapeleka katika lugha ya Kiingereza ni kuwachanganya zaidi. Katika shule moja iliyopo Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, baadhi ya wanafunzi hawakusita kueleza hisia zao za kuacha shule kwa sababu ya kushindwa kuelewa Kiingereza.

Tanzania haipaswi kusita kufanya uamuzi juu ya jambo hili ili kuwajengea wanafunzi msingi mzuri katika usomaji wao. Katika mazingira ya sasa, asilimia kubwa ya wazazi huwapeleka watoto wao katika shule zinazofundisha Kingereza na Kiswahili kama
somo la ziada.

Katika mazingira ya uswahilini, watoto wanaosoma shule hizo huonekana daraja la kwanza na wale wanaosoma shule za
kawaida, huonekana daraja la pili.

Jambo hilo ni la kisera na linahitaji wakati, fedha na rasirimali watu lakini lisiwe jambo la kuugopa kwani kila jambo hupangwa na binadamu na ndiye anayeweza kutekeleza kwa sababu fulani.

Katika mazingira hayo, Tanzania inapaswa kufanya mabadiliko ya  mfumo huo ili uweze kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri zaidi kwa ajili ya kuijenga Tanzania bora kielimu.

No comments:

Post a Comment