10 December 2012

Miaka 51 ya Uhuru, tukomeshe mimba kwa wanafunzi wa kike



RAIS Jakaya Kikwete jana alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 51 ua Uhuru wa Tanzania Bara.

Katika maadhimisho hayo, Rais Kikwete alisema Tanzania
inajivunia maendeleo lukuki yaliyoletwa na Serikali ya chama
tawala katika nyanja mbalimbali, amani na utulivu tulionao.


Pamoja na mafanikio hayo, changamoto ni nyingi katika baadhi
ya maeneo hususan katika sekta ya elimu ambayo ndio ufungua
wa maisha na nguzo ya maendeleo yoyote duniani.

Wakatio tukiadhimisha miaka 51 ya uhuru wa Tanzania Bara, tatizo  la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini, linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu.

Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinathibitisha kuwa tatizo hili limekuwa likiongezeka siku hadi siku hasa baada
ya kuanzishwa shule za kata.

Pamoja na shule hizo kupunguza tatizo la wanafunzi kukosa nafasi za masomo, bado zinakabiliwa na changamoto nyingi.

Miongoni mwa changamoto hiyo ni wanafunzi wa kike kupewa mimba hivyo wengi wao hulazimika kukatisha masomo, uhaba
wa vifaa, vyumba vya madarasa, walimu na madawati.

Tafiti mbalimbali zimebaini kuwa, tatizo la mimba kwa wanafunzi hasa wa sekondari ni kubwa na linagusa hisia za kila mpenda maendeleo.

Jambo la kusikitisha jamii kubwa bado haijahamasika kutoa ushirikiano wa karibu kwa vyombo vya dola ili kuwafichua wahusika wa vitendo hivyo.

Baadhi ya wazazi hupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa ili wasifikishwe katika vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua stahiki ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia za aina hiyo.

Sisi tunasema dhamira yetu ni kuona wazazi wanashirikiana na vyombo hivyo kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Kama jamii itaona umuhimu huu, Tanzania yenye wasomi wazuri waliobobea katika fani mbalimbali itawezekana na maendeleo yatakuwa kwa haraka.

Kitendo cha jamii kuendelea kuwaficha wahusika wa vitendo hivi, kinarudisha nyuma juhudi za Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora.

Umefika wakati wa wanafunzi wa kike kupewa elimu ya kujitambua ili waweze kufahamu wajibu walionao kwa jamii na Taifa. Hali hiyo itawafanya wajiepushe na vishawishi vinavyoweza kusababisha wapate mimba au kuacha shule.

Elimu ni nyenzo muhimu kwa maendelo ya Taifa lolote duniani kwani mapinduzi mengi ya maendeleo, hutegemea kiwango cha elimu kwa jamii husika.

No comments:

Post a Comment