18 December 2012
Kombani: Watumishi walevi wachukuliwe hatua
Na Pendo Mtibuche, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Celina Kombani, amewaagiza wakuu wa idara za utawala na utumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa,
kuwachukulia hatua watumishi walevi kupindukia, wajeuri,
wazembe, mafisadi, washerati, wasumbufu, wala rushwa na
wale wanaotumia madaraaka yao vibaya.
Bi. Kombani alitoa agizo hilo mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano wa mwakla wa wakuu wa idara za utawla na utumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Alisema hivi sasa kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni, taratibu na miiko ya kazi katika utumishi wa umma kama ulevi
wa kupindukia na dharau kwa wananchi ambao ndio walipa kodi.
Aliongeza kuwa, vitendo hivyo ni sehemu ya mambo yanayofanyika katika Serikali za Mitaa na mengine mengi ambayo wanafanyiwa wananchi wanapokwenda kupata huduma lakini wakuu wa idara wanayafumbia macho bila kuchukua hatua zozote.
“Katika baadhi ya hospitali zetu wagonjwa wanatolewa kauli chafu hususan wanawake wanaokwenda kujifungua, majibu ya barua mbalimbali yanachelewa kutolewa lakini bado unafumbia macho, sasa nataka muanze kuchukua hatua,” alisema.
Alisema utumishi wa umma katika mamlaka hizo unakabiliwa na changamoto ya maofisa husika (wakuu wa idara za utawala na utumishi), kutozingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo
wanaposhughulikia masuala ya kiutawala na kiutumishi.
Aliongeza kuwa, hivi sasa baadhi ya maofisa hao hawafuati sheria ya utumishi wa umma namba 8 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni
za utumishi wa umma za 2003 wanaposhughulikia nidhamu.
Kutokana na hali hiyo, watumishi wengi wanaosimamishwa kazi wamekuwa wakishinda kesi mahakamani hivyo Serikali kuingia hasara ya kuwalipa fidia na usumbufu.
“Ukiukwaji wa taratibu katika kuendesha mashauri ya kinidhamu, yamekuwa yakiisababishia Serikali kutumia muda mrefu kuendesha kesi na kuendelea kuwalipa mishahara watumishi waliosimamishwa na kurudishwa kazini wanaposhinda kesi zao,” alisema.
Akizungumzia changamoto ya upungufu wa wataalamu katika fani mbalimbali, Bi. Kombani alisema watumishi wengi wanapangwa maeneo ya mijini hivyo kuathiti utoaji huduma vijijini.
Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza maofisa hao kuhakikisha halmashauri zote zilizojaza watumishi mijini, zinawapeleka
vijijini ili kuweka uwiano ulio sawa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hab Mkwizu, alisema kuwa tathimini zinazofanywa na ofisi yao zinaonyesha rasilimali watu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa bado ni tatizo.
“Masuala mengi ya kiutawala na kiutumishi, bado yanashughulikiwa bila kuzingatia taratibu za kisheria, kanuni na miongozo iliyopo hivyo kusababisha matatizo mbalimbali kwa watumishi, kukosa
stahili zao na kuongezeka malalamiko.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment