18 December 2012
Kamati ya siasa yajadili mgogoro wa Balozi Kagasheki, Dkt. Amani
Na Livinus Feruzi, Bukoba
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Bukoba Mjini, mkoani Kagera, imelazimika kuitisha kikao cha dharura ili kujadili hali ya kisiasa jimboni humo.
Katika kikao hicho, wajumbe wote walitakiwa kuzima simu zao
za mkononi ili wasiweze kuvujisha siri za mkutano huo.
Mkutano huo ulifunguliwa na Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Bukoba Mjini, Bw. Yusuph Ngaiza, ambapo kati ya washiriki wa mkutano huo ni pamoja na Mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki na Meya ya Manispaa hiyo, Dkt. Anatory Amani.
Ajenda za mkutano huo zilikuwa kujadili hali ya kisiasa jimboni humo, utekelezaji wa miradi ya halmashauri na kufanya tathimini
ya chaguzi za jumuiya ambapo Bw. Ngaiza alisema, asingependa mazungumzo ya kikao hicho yarekodiwe.
Alisema sababu ya kufanya hivyo ni kutokana na kikao hicho kuwa cha ndani akitolea mfano wa mkutano CCM uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni ambapo wajumbe walilazimishwa kuzima
simu zao ili siri za mkutano zisitoke kabla mkutano haujaisha.
“Tumekutana hapa kujadili na mstakabari wa chama chetu hivyo tusingependa mtu arekodi mazungumzo haya, sisi sote ni baba mmoja hivyo tuzungumze kwa pamoja,” alisema Bw. Ngaiza.
Bw. Ngaiza alikiri kuwepo kwa mpasuko uliotokana na mgogoro wa kisiasa uliopo kati ya Balozi Kagasheki na Dkt. Amani juu ya ujenzi wa soko jipya la kisasa.
“Tunakaa kikao hiki kutokana na agizo la Kamati ya Siasa ya
CCM Mkoa, ambayo katika kikao chao walijadili mgogoro huu
na kutuagiza tukae vikao vya kikatiba haraka iwezekanavyo.
“Kamati husika ilitutaka tujadili hali iliyojitokeza na kuwasilisha mapendekezo ngazi ya Mkoa kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu kabla haujaleta madhara makubwa zaidi,” alisema.
Mgogoro uliopo kati ya Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri
wa Maliasili na Utalii na Dkt. Amani, unatokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na manispaa hiyo.
Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa soko la kisasa unaopingwa na Balozi Kagasheki ambaye anadai mkataba wa ujenzi huo unafanywa siri wakati utekelezaji wa mradi huo ni moja ya ahadi za mbunge alizozitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu 2010.
Kutokana na hali hiyo, hivi karibuni Mkurugenzi wa manispaa
hiyo Bw. Khamis Kaputa, alikutana na waandishi wa habari na
kudai kuwa, halmashauri haijaingia mkataba wa ujenzi wa soko
kwa sababu mchakato wa upembuzi yakinifu haujafikia hatua ya
kutangaza zabuni ya ujenzi.
Halmashauri hiyo inatekeleza miradi mbalimbali ambayo baadhi yake ni mradi wa viwanja 5,000, ujenzi wa soko la kisasa, kitega uchumi na ujenzi wa kituo cha mabasi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment