05 December 2012
Halmashauri yavunja ukimya ujenzi soko la kisasa Bukoba
Na Livinus Feruzi, Bukoba
BAADA ya mvutano mkali kati ya Mbunge wa Bukoba Mjini, mkoani Kagera, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa
ya Bukoba, Dkt. Anatory Amani, juu ya ujenzi soko jipya la kisasa, halmashauri ya manispaa hiyo imeamua imeamua kuvunja ukimya.
Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bw. Khamis Kaputa, alisema ujenzi wa soko hilo utaanza baada ya taratibu muhimu kukamilika na kudai hakuna mzabuni aliyeingia mkataba na halmashauri.
Alisema halmashauri hiyo haijaingia mkataba wowote wa ujenzi wa soko hilo kama ilivyodaiwa na baadhi ya watu kwani mchakato wa upembuzi yakinifu haujafikia hatua ya kutangaza zabuni ya ujenzi.
Ufafanuzi huo wa Serikali umetokana na agizo la hivi karibuni ambalo limetolewa na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo.
Kamati hiyo iliitaka Manispaa ya Bukoba kutoa taarifa sahihi juu ya utekelezaji mradi huo ili kuondoa wasiwasi uliojengeka miongoni mwa jamii ambapo Bw. Kaputa alisema mchakato wa upembuzi yakinifu bado unaendelea kufanyika.
“Ujenzi wa soko hili ni utekelezaji wa moja ya ahadi za Balozi Kagasheki alizozitoa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010,
hadi sasa manispaa haijaingia mkataba wa ujenzi wa soko hili
kwa sababu upembuzi yakinifu haujatufikisha katika hatua ya kutangaza zabuni ya ujenzi,” alisema.
Hata hivyo, kauli ya Bw. Kaputa inapingana na na ile iliyotolewa
na Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye hivi karibuni akiwa katika mkutano wa hadhara, alidai uongozi wa halmashauri hiyo unaufanya siri mkataba huo wa
ujenzi wa soko hilo.
Balozi Kagasheki alisema kutokana na hali hiyo, soko hilo halitafunjwa ili kupisha ujenzi wa kisasa hadi atakapooneshwa mkataba huo pamoja na kupata muafaka wa wafanyabiashara waliomo katika soko.
Bw. Kaputa alisema hatua zilizochukuliwa hadi sasa ili kufanikisha ujenzi huo ni pamoja na kujua maeneo ambayo watawapeleka wafanyabiashara ambao hivi sasa wapo katika soko hilo.
Maeneo hayo ni jengo la CCM mkoani humo, Soko la Nyakanyasi, machinjio ya zamani na eneo la chama hicho Kata ya Miembeni.
Alisema awali tenda ya ujenzi wa soko hilo ilipaswa kutangazwa Aprili mwaka huu na kutolewa Juni ili ujenzi rasmi wa soko uanze Septemba lakini walichelewa kutokana na sababu mbalimbali.
Miongoni mwa sababu hizo ni kuchelewa kwa mkandarasi mshauri kuchukua vipimo vya udongo na kikundi cha wafanyabiashara kufungua kesi mahakamani ya kupinga kuondolewa sokoni hapo.
Akizungumzia tuhuma za kuficha mikataba ya ujenzi wa soko hilo, Bw. Kaputa alisema mikataba ya halamshauri ni ruksa kukaguliwa na mtu baada ya kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi.
Manispaa hiyo inatekeleza miradi mbalimbali ukiwemo wa viwanja 5,000, ujenzi wa soko la kisasa, kituo cha mabasi, kitega uchumi na mradi wa kuosha magari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment