05 December 2012
Mgogoro wa Chasimba sasa wapatiwa tiba
Na Rachel Balama
WAKAZI wa eneo la Chasimba, Kata ya Bunju na Wazo, wamekubali ombi la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka, kuruhusu eneo la mgogoro kati yao na kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill kupimwa.
Pia wakazi hao wamekubali eneo hilo lifanyiwe tathmini ila watendaji wote waliohusika kutoa vilelelezo feki na kusababisha wao kushindwa kesi mahakamani waondolewe.
Hatua hiyo ilifikiwa jana katika mkutano wa pamoja kati ya Prof. Tibaijuka na wananchi hao uliokuwa na lengo la kujadilinini cha kufanya ili mgogoro huo uweze kupatiwa ufumbuzi.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao, Diwani wa Kata ya Bunju Majisafi Sharifu, alisema wananchi wapo tayari kwa hatua hiyo lakini ni vyema watendaji wote walioshiriki kutoa vielelezo feki ambavyo vipo wizarani na kusababisha wao kushindwa kesi washughulikiwe.
Alisema kutokana na ubabaishaji uliofanywa na watendaji ambao si waaminifu, ndio waliosababisha tatizo hilo kufika hapo lilipo.
Akijibu hoja hiyo, Prof. Tibaijuka aliwaahidi wananchi hao na kudai yupo tayari kuwashughulikia watendaji hao kama watabainika walichakachua baadhi ya nyaraka.
“Nawaahidi kwamba suala lenu nimelipokea nitalishughulikia na kuhakikisha watendaji wote walisababisha mgogoro huo kufikia hapo ulipo kwa kuchakachua vielelezo mwisho wao leo,” alisema.
Alisema hana tatizo na wananchi hao kuwepo maeneo hayo kwa kuwa si makosa yao bali ya viongozi kwani wakati wananchi wanajenga hawakutoa tahadhari kwamba eneo hilo haliruhusiwi.
Hata hivyo, Prof. Tibaijuka alisema Serikali italipima eneo hilo ili kujua ukweli na baada ya kupima, watafanya tathmini na kadiri hatua hizo zitakapofanyika watapewa taarifa.
Aliwataka wananchi hao kujaza dodoso ambalo litapita kwa
lengo la kuisaidia Serikali ili kufanikisha azma yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment