05 December 2012
Tanzania yaongoza kwa chakula EAC
Na Mariam Mziwanda
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Chakula, Mhandisi Mbogo Futakamba, amesema Tanzania inaongoza kwa kuwa na
chakula katika nchi za Afrika Mashariki.
Alisema hadi sasa ina uwezo wa kuzalisha chakula asilimia 113 tofauti na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Mhandisi Futakamba aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa, hiyo ni hatua nzuri katika uzalishaji mazao ya chakula hivyo hakuna mwananchi ambaye ataweza kufa na njaa.
Alisema katika maeneo yenye njaa nchini, hali hiyo inachangiwa
na ujanja wa baadhi ya wafanyabiashara ambao hupandisha bei
ya bidhaa kwa masilahi yao binafsi.
“Sisi hatukatai kama hali ya uzalishaji inatofautiana katika mikoa, ukweli ni kwamba katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania inajitahidi kuzalisha tofauti na nchi nyingine,” alisema.
Akizungumzia ziara ya wakulima na wafanyabiashara 17 ambao wamekwenda nchini Sudai Kusini, Septemba mwaka huu, katika maonesho ya wakulima na wafanyabiashara nchini humo, alisema wamejifunza mambo mengi na kubaini changamoto.
“Wamebaini changamoto nyingi zinazochangia kuwakwamisha wakulima na wafanyabiashara wengi nchini kwetu, kukosekana
kwa balozi anayeiwakilisha Tanzania nchini humo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo, matatizo mbalimbali yanayowakabili Watanzania na wafanyabiashara waliopo Sudan Kusini,
yanatatuliwa na Ubalozi wa Kenya,” alisema.
Alisema wakulima hao wamebaini bidhaa nyingi za Tanzania ambazo zinasafirishwa kwenda nchini humo zinahujumiwa kwa kubandikwa nembo ya nchi nyingine na kuuzwa kwa bei ya juu jambo ambalo linawanufaisha watu wengine.
Aliongeza kuwa, uchumi wa Sudani Kusini ni tegemezi kwa nchi
nyingine ambapo nchi hiyo ni Taifa changa ambalo limepata uhuru wake Julai 9,2011 lakini amefurahishwa na Tanzania kung'ara katika maonesho hayo.
“Nchi hii imeonesha nia ya kutaka kujifunza mambo mbalimbali nchini kwetu hasa katika sera za kilimo na uwekezaji,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, Bi. Betty Mkwasa
ambaye naye alikuwa miongoni mwa waliofanya ziara hiyo, alisema ni vyema Serikali ikafanya jitihada za kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara kufika nchini humo kwa urahisi tofauti na sasa.
Mkulima Aquiline Francis kutoka mjini Bukoba, mkoani Kagera, ambaye alikuwa miongozi mwa wasafiri hao, alisema akulima nchini humo hawajajipanga katika kilimo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment