24 December 2012

Dhana ya kujitegemea itachochea maendeleo


WAKATI hayati Mwalimu Julius Nyerere, akijenga misingi ya kukuza uchumi wa Tanzania baada ya uhuru, alitangaza siaasa
ya ujamaa na kujitegemea.


Mwalimu aliamini kuwa, kutokana na nguvu za Watanzania wenyewe bila kutegemea misaada kutoka nje, Tanzania itapiga
hatua ya maendeleo kwa haraka hivyo kukidhi mahitaji ya
wananchi wake na kukuza uchumi.

Kutokan na imani hiyo, Mwalimu alihamasisha matumizi ya rasilimali za ndani ili kujenga nchini na kupinga kwa nguvu
zote misaada kutoka nje akiamini inachangia kudumaza
maendeleo na fikra za Watanzania.

Chini ya mtazamo huo, miaka michache baada ya uhuru Tanzania ilipiga hatua kubwa ya maendeleo. Ilianzisha viwanda mbalimbali kikiwemo cha zana za kilimo na kuwa juu kiuchumi miongoni
mwa nchi za nyingi za Afrika Mashariki.

Hivi sasa, viongozi wengi nchini wameacha kuhamasisha moyo wa kujitegemea. Sisi tunaamini kuwa, dhana ya kujitegemea bado ina umuhimu mkubwa kwa Watanzania hata kama sera ya ujamaa imepitwa na wakati.

Upo umuhimu mkubwa wa viongozi kuhubiri dhana hii badala ya kugeuka mabingwa wa kuhangaika kutafuta wafadhili ili kuomba misaada.

Hivi sasa jamii kubwa inaamini kuwa, kiongozi bora ni yule anayekwenda kwa wafadhili kuomba misaada ya kuipeleka kwao.

Mfano mzuri ni namna wabunge wetu wanavyohangaika kutafuta misaada ya kila aina kupeleka majimboni kwao.

Anayepeleka misaada jimboni, anaonekana anafanya kazi nzuri hivyo kupewa nafasi kubwa ya kuchaguliwa tena.

Wajibu wa kiongozi hasa mbunge sio kuhangaika kutafuta misaada kwa kuombaomba kwani dhana hiyo ndio aliyoikataa Mwalimu bali jambo la msingi ni kuwajengea wananchi moyo wa kujitegemea.

Imani yetu ni kwamba, jukumu moja wapo la mbunge ni kuhamasisha, kuandaa na kusimamia wananchi wake ili waweze kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali chache walizonazo.

Kwa kufanya hivyo, watasaidia kupatikana maendeleo endelevu ambayo yatawasaidia kubadilika kifikra.

1 comment:

  1. HAKUNA SERA YA TAIFA KUNA VYAMA VINAVYOHAMASISHA WANANCHI WASIJITOLEE NINI WANALIPA KODI UKIWAULIZA WAMELIPA TSHS NGAPI WANAKAZA MISHIPA YA SHINGO BILA JIBU LINALOELEWEKA LABDA WAFANYAKAZI NDIO WANAOKATWA VAT KWENYE MISHAHARA YAO HII NCHI NI BORA LIENDE NI KICHWA CHA MWENDAWAZIMU CHA KUJIFUNZIA KUNYOA MCHAWI WA MAENDELEO YETU NI SISI WENYEWE INGAWA NA SERA CHAFU ZA IMF NA WORLD BANK

    ReplyDelete