18 December 2012
Apanda nguzo ya umeme na kusababisha taharuki
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
MKAZI wa Kijiji cha Butulwa, Kata ya Old Shinyanga, Bw. Shija Machiya (30), jana alisababisha taharuki kubwa baada ya kupanda katika nguzo inayopeleka umeme kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, wilayani Kahama.
Tukio hilo lilisababisha baadhi ya watu kuacha shughuli zao katika eneo la Ihapa na kumshangaa kijana huyo na kuhofia usalama wa maisha yake.
Akizungumza na gazeti hili, mama mzazi wa kijana huyo Bi. Mondesta Madirisha, hali hiyo ilitokana na mtoto wake kuchanganyikiwa baada ya kupata ugonjwa wa malaria.
“Tulimpa dawa ya kienyeji na hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri lakini jana saaa mbili asubuhi, hali ilibadilika ghafla na kuanza kupiga kelele, alitoroka nyumbani na kukimbia ovyo barabarani
hivyo baadhi ya watu walianza kumfuatilia.
“Leo asubuhi (jana), wakati nikitoka shambani, ghafla nilikutana naye akikimbia, nilimsemesha na kumuomba asimame akagoma hivyo niliwaomba watu wanisaidie kumkamata lakini aliwazidi
mbio na kupanda kwenye nguzo ya umeme,” alisema.
Alisema baada ya kuona hivyo, waliamua kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali ya kitongoji na kijiji ambao walichukua hatua za kuwaarifu wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), ambao walifika eneo hilo, kuwasiliana na polisi pamoja Kikosi cha Zimamoto.
Kijana huyo aliteremshwa kutoka juu ya nguzo hizo mbali ya kujaribu kuwachenga akiwa amevua nguo zake lakini watu waliopanda kumshusha walifanikiwa kumkamata.
Kwa upande wake, Mhandisi wa njia kuu za umeme mkoani humo, Bw. Job Bidya, alisema kitendo cha kijana huyo kupanda katika nguzo yenye umeme mkubwa KV 220, kingeweza kuhatarisha maisha yake.
“Baada ya kupata taarifa na kufika eneo la tukio, tulilazimika kuzima umeme haraka, juhudi za kumteremsha zilifanyika kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Manispaa ya Shinyanga, Jeshi la Polisi na wananchi,” alisema.
Jeshi la Polisi mkoani humo limethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo kijana huyo wanamshikilia kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini kaama alifanya kitendo hicho kwa makusudi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment