21 November 2012

Zitto alipuka tena sakata la ufichaji fedha UswisiNa Angelina Faustine

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Bw. Kabwe Zitto, amepingana na kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Bw. George Mkuchika kuwa, Serikali ya Uswisi imeitaka Tanzania kupeleka majina ya watu wanaotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo kama sharti la kusaidia uchunguzi wa tuhuma hizo.


Bw. Kabwe aliyasema hayo Dar es Salam jana katika taarifa
 yake kwa vyombo vya habari na kusisitiza kuwa, Serikali
inapaswa kutekeleza Azimio la Bunge badala ya kutoa
kauli tata za kukata tamaa.

Alisema suala la Serikali ya Uswisi kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akichangia hoja binafsi ambayo aliiwakilisha bungeni na wakati akipeleka maombi yake
ya kuiondoa hoja ambayo yalikataliwa na Bunge.

Aliongeza kuwa ni wazi Serikali inajihami kwa kuona kama itashindwa kutekeleza Azimio la Bunge, hivyo Watanzania wasikubali propaganda hiyo.

“Bunge limeiagiza Serikali ifanye uchunguzi kwa kutumia njia za kiserikali au wachunguzi binafsi wa kimataifa, kwanini Serikali inaanza kubwabwaja wakati hawajaanza kuifanya kazi hiyo, inajaribu kuficha nini.

“Watanzania wanapaswa kujua kwamba, Taifa la Uswisi limejengwa na linajengwa kwa fedha hizi ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa kodi kwenye nchi zao na kuzificha huko, alisema Bw. Kabwe.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Uswisi hata siku moja haiwezi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika suala kama hilo ndio maana Azimio la Bunge linataka wachunguzi binafsi ambao hawatahitaji ushirikiano wa Serikali hiyo.

“Mwaka 1997 mara baada ya Joseph Desire Mobutu kuangushwa na Rais Joseph Kabila nchini Congo, Serikali ya Uswisi iliitaka Serikali ya nchi hiyo kuonesha ushahidi wa fedha za Mobutu zilipatikana kwa njia haramu.

“Waswisi walimtaka Rais Kabila awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola bilioni nane za Marekani hazikupatikana kihalali ili wazirudishe, nchi hiyo ilikadiriwa kuwa na zaidi ya dola za Marekani bilioni 30 katika benki zilizopo nje ya nchi hiyo,” alisema.

Aliongeza kuwa, majibu ya aina hiyo hutolewa kwa nchi mbalimbali hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao walijibiwa hivyo hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua taarifa hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi.

Alisema lihoji kwanini Serikali ya Tanzania ishabikie majibu yao na kusahau historia kwa haraka zaidi badala ya kuchunguza utoroshaji wa fedha haramu na kutoa taarifa bungeni.

“Serikali ya Tanzania inapaswa kuanza uchunguzi mara moja kama ilivyoelekezwa na Bunge, suala hili si la kisiasa ni Azimio la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa kikamilifu.

“Suala hili si la Zitto Kabwe tena bali la Bunge na wananchi, kama hawawezi wapishe watu wenye uwezo wa kusimamia masilahi ya Watanzania kwa kuchukua hatua stahili za kuchunguza utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni, ukwepaji mkubwa kodi na ufisadi uliosababisha kufichwa mabilioni nje ya nchi yetu,” alisema.

Aliongeza kuwa, utekelezaji wa Azimio la Bunge ni salamu tosha kwa mafisadi na watoroshaji fedha haramu kuwa hawana pa kujificha kwani Tanzania si Taifa la kuchezea chezea hivyo
lazima tushinde vita hiyo.

Bw. Kabwe alisema anayeona hawezi kutuongoza kuishinda vita hiyo aondoke mapema kwani Watanzania si mabwege tena.

1 comment:

  1. ZITTO KUMBE UNAELEWA UGUMU WA KESI HIYO KUICHAGIZA SERIKALI IINGIE MKENGE JE IKIKOSA USHAHIDI WAKATI IMESHIKIANA NA WEWE KUTATA WATU UKO TAYARI KULIPA FAINI KUWASAFISHA TUNAOMBA IWAPO HUNA USHAHIDI WATANZANIA KODI ZETU ZISITUMIKE KULIPA FAINI KAMA VILE TUNALIPIA MITAMBO YA UMEME AMBAYO TUMEKODI YA SIMBION WAKATI HAIZALISHI UMEME TUNAFAHAMU UATAKA KUJIJENGEA UMAARUFU WEWE NA LIPUMBA SIO KUPITIA MIGONGONI MWA WATANZANIA MASKINI

    ReplyDelete