21 November 2012

Uamsho Z'bar washauriwa kufungua kesi




Na Mohammed Mhina, Jeshi la Polisi Zanzibar

MAHAKAMA Kuu ya Vuga mjini Zanzibar, jana imetoa ushauri kwa viongozi wa Jumuiya mbili za Kiislamu visiwani humo ambao wanakabiliwa na makosa ya kuhatarisha usalama wa Taifa na kudai kama hawajatendewa haki gerezani wafungue kesi ya madai.


Ushauri huo umetolewa na Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Bw. George Kazi, baada ya kupitia maombi ya washtakiwa ambayo  yalifikishwa kwake Novemba 8 mwaka huu, kupitia mawakili wao.

Kesi hiyo inawakabili watu wanane akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar Shekhe Faridi Hadi Ahmedi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho Shekhe Mselem Ali Mselem.

Wengine ni Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman
na Ghalib Ahmada Omar.

Akitoa uamuzi huo, Bw. Kazi alisema washtakiwa wana haki
ya kufungua kesi Mahakama Kuu juu ya kile wanacholalamikia
kwani mahakama hiyo itakuwa na uamuzi wa kuyasikiliza madai yao tofauti na kesi ya msingi inayowakabili.

Kupitia kwa mawakili wao, washtakiwa hao walidai  kunyimwa uhuru, haki zao za msingi pamoja na kupigwa marufuku kufugaji
ndevu wakiwa rumande katika Chuo cha Mafunzo.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne yakiwemo ya kutoa lugha za uchochezi, kufanya vurugu na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara mjini Zanzibar.

Wakizungumzia kesi ya msingi kwa washtakiwa hao, Waendesha Mashtaka wa Serikali walidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamili
hivyo waliomba siku hiyo ipangwe siku nyingine.

Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Bw. Kazi aliihairisha
hadi Novemba 29 mwaka huu, itakapotajwa tena.

Jeshi la Polisi lilifunga barabara zote za kuingia na kutoka mahakamani ili kuimarisha ulinzi ndani na nje ya mahakama
hiyo ambapo kila pembe walionekana makachero wa polisi na
 askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Baadhi ya wananchi waliofika makahakamani hapo waliwaomba waandishi wa habari kuandika ukweli kuhusu kesi hiyo ili kuinusuru nchi isikumbwe na machafuko.

Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Bw. Salum Toufik na Bw. Abdallah Juma Kaka, wakati upande wa Serikali unawakilishwa na Bw. Ramadhani Nassibu na wenzake wawili kama Waendesha Mashtaka.

No comments:

Post a Comment