21 November 2012

SAKATA MFUNGWA WA SMG Polisi kuanika kila kitu leo


Na Suleiman Abeid, Shinyanga

JESHI la Polisi mkoani Simiyu, limekanusha madai ya Jeshi la Magereza kuwa mfungwa aliyehukumiwa miaka 15 mwaka 2010, Bw. Masanja Maguzu (42), alikamatwa uraiani akiwa silaha za kivita baada ya kumaliza kifungo chake gerezani.

Bw. Maguzu alikamatwa hivi karibuni nyumbani kwake Kijiji cha Ng’wang’wali, Wilaya ya Itilima, akiwa na bunduki aina ya SMG, risasi 31 na magzini tatu ambazo kati ya hizo, moja hutumika kwenye bunduki aina ya Uzi Gun, iliyotengenezwa Israel.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Salum Msangi, alisema kwa mujibu wa kumbumbu za ofisi yake, muda wa mfungwa huyo kutumikia adhabu gerezani bado haujamalizika.

Alisema Bw. Maguzu alihukumiwa kifungo hicho mwaka
2010 baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani
Shinyanga, kumtia hatiani kwa makosa manne.

Aliongeza kuwa, kutokana na uzito wa makosa yaliyomtia hatiani, kwa mujibu wa sheria mfungwa huyo haruhusiwi kupewa msamaha wa Rais hivyo taarifa zinazodai alikuwa akitumikia ya kifungo cha miaka mitano gerezani kama ilivyotolewa ufafanuzi wa Jeshi la Magereza, muda huo bado haujamalizika.

Kamanda Msangi alisema, mfungwa huyo alihukumiwa kifungo
cha miaka 15 gerezani baada ya yeye na mwenzake Bw. Japheth Sylvester kutiwa hatiani na mahakama kwa kosa la kupatikana na bunduki aina Sub Machine Gun (SMG), risasi 622, nyara za Serikali (nyama ya nyati) wakiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Hata hivyo, Kamanda Msangi alisema leo ofisi yake itatoa tamko rasmi kuhusu sakata la mfungwa huyo kukamatwa na silaha za
kivita akiwa uraiani baada ya kufanya naye mahojiano ya awali.

“Nitaeleza ukweli wote jinsi mfungwa huyu alivyoweza kutoka gerezani na kumwacha mwenzake, sisi tulimkamata kwa mara nyingine Novemba 16 mwaka huu,” alisema.

Mfungwa huyo alikamatwa siku 10 baada ya Jeshi la Polisi mkoani humo kumkamata mkewe, Bi. Holo Mabuga (30) akiwa na silaha nyingine ya kivita aina ya G. 3 na risasi 36 kinyume cha sheria.

Hali hiyo iliwafanya polisi kuwa na wasiwasi wakiamini kuwa, mwanamke huyo asingeweza kutumia silaha hiyo peke yake hivyo waliweka mtego ili kuubaini mtandao ambao unashiriiaana naye kufanya vitendo vya uhalifu na kufanikiwa kumkamata mfungwa huyo akiwa na silaha nyingine.

Gazeti moja linalotoka kila siku, jana lilimnukuu Msemaji wa Jeshi la Magereza, Bw. Omary Mtinga ambaye alidai kuwa, mfungwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka mitano si 15 kama walivyodai Jeshi la Polisi.

Alisema mfungwa huyo hadi anakamatwa alikuwa tayari amemaliza kifungo chake baada ya kukutwa ndani ya hifadhi ambapo Mahakama ilimkuta na makosa matatu kati ya hayo, mawili alishinda na moja la kukutwa ndani ya hifadhi ndilo lililomfunga. 

No comments:

Post a Comment