28 November 2012

Wakazi wa Dar wakamatwa na dawa za kulevya Z'bar


Na Mohammed Mhina, Jeshi la Polisi Zanzibar

WAFANYABIASHARA wawili wakazi wa Dar es Salaam, wametiwa mbaroni visiwani Zanzibar baada ya kukamatwa wakiingiza dawa za kulevya kwa njia ya majini.

Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, ACP Yusuf Ilembo, amewataja watuhumiwa hao ni Bw. Othuman Chande Othmani (22), mkazi wa Kinondoni na Bw. Abubakari
Muharami Bakari (33), mkazi wa Temeke.

Kamanda Ilembo alisema, watuhumiwa hao walikamatwa katika Bandari ya Zanzibar baada ya kuwasili kwa boti wakitokea Dar
es Salaam wakiwa na dawa hizo aina ya heroine.

Alisema mtuhumiwa Bw. Bakari alikamatwa juzi saa tatu asubuhi akiwa na kifurushi kimoja likichokuwa na dawa hizo ambapo Bw. Othman, alikamatwa jana saa tatu asubuhi akiwa na vifurushi
viwili vya dawa hizo.

Aliongeza kuwa, kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na kuimarishwa kwa ulinzi na upekuzi wa hali ya juu uliopo katika maeneo ya Viwanja vya Ndege na Bandari ya Zanzibar.

“Watuhumiwa hawa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kupatikana na dawa hizi, nawaomba wananchi, wasafiri ambao wanatumia ndege na boti kuingia visiwa vya Unguja na Pemba, wasilalamike pale nawapopekuliwa,” alisema.

Mbali ya dawa ya kulevya na silaha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pia imepiga marufuku uingizwaji mifuko ya plastiki ya aina zote na mtu yeyote ambaye atapatikana na mifuko hiyo atakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Hivi karibuni, baadhi ya wasafiri wamekuwa wakilalamikia upekuzi unaofanywa katika maeneo ya Viwanja vya Ndege, Bandari na kuona hali hiyo ni usumbufu mkubwa kwao.

No comments:

Post a Comment