28 November 2012

Mnyika aivaa serikali, wabunge CCM


Na Daud Magesa, Mwanza

MBUNGE wa Ubungo, Bw. John Mnyika, amesema umaskini uliopo nchini umetokana na udhaifu wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na wabunge wa chama hicho.


Bw. Mnyika aliyasema hayo akiwa katika Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Nilipokuwa bungeni mjini Dodoma, niliwahi kusema tumefika hapa tulipo kutokana na udhaifu wa Rais Jakaya Kikwete, uzembe wa Bunge na ulegelege wa CCM, nikaambiwa niifute.

“Nilitumia kauli ya Hayati Mwalimu Nyerere katika kitabu cha uongozi wetu wa sasa na hatma ya nchini yetu, ambacho aliandika kuwa, chama legelege huzaa serikali legelege,” alisema.

Aliongeza kuwa, kama Serikali ya CCM ingekuwa imara na wabunge wa chama hicho kutetea masilahi ya nchi, tusingefika
hapa tulipo lakini kuokana na ulegelege na dhaifu huo, ndio
chanzo cha madudu yanayofanywa na watendaji wake bila
wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria au kuwajibishwa.

Alisema ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge ndicho chombo cha kuishauri na kusimamia Serikali hivyo kitendo cha Mawaziri kusimamiwa na NEC ya
CCM ni uzembe wa wabunge wa chama hicho kushindwa kuibana Serikali yao.

“Tiba pekee ya kuondoka katika hali tuliyonayo ni wananchi  kufanya mabadiliko sahihi ili nchi ipate chama mbadala, kiongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganaizesheni thabiti,” alisema.

Bw. Mnyika alisisitiza kuwa, haoni sababu ya NEC ya CCM kumsaidia Rais Kikwete kwa kushindwa kuisimamia Serikali yake, bali kinachotakiwa na Rais kuchukua hatua na maamuzi magumu.

No comments:

Post a Comment