28 November 2012

Jerry Muro kortini tena *Kesi aliyoshinda kusikilizwa upya Mahakama KuuNa Rehema  Mohamed

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo inatarajiwa
kuanza kusikiliza rufaa ya Serikali dhidi ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji nchini (TBC1), Bw. Jerry Muro na wenzake.

Kwa mujibu wa wakili wa utetezi, Bw. Richard Rweyongeza, alisema rufaa hiyo inatarajiwa kusikilizwa mbele ya Jaji Dkt.
Fauz Twaib wa Mahakama hiyo.

Katika rufaa hiyo, upande wa Serikali unapinga hukumu iliyotolewa na Hakimu Frank Moshi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambayo iliwaachia huru Bw. Muro na wenzake
kwa madai kuwa, upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Hakimu Moshi alidai vidhibiti vilivyofikishwa mbele ya Mahakama hiyo na upande wa mashtaka vilikuwa haviendani na kesi hiyo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa Bw. Edmund Kapama na Bw. Deogratius Mugasa, ambao kwa mara ya kwanza
walifikishwa Mahakamani Februari 5,2011.

Mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili ni kula njama na kuomba rushwa ya sh. milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, Bw.
Michael Wage.

Wakati shauri hilo likisikilizwa upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi saba pamoja na vielelezo, ambapo inadaiwa kuwa, Januari 28,2011 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikula
njama ya kutenda kosa la kuomba rushwa.

Katika shtaka la pili ilidaiwa Januari 29,2011, kwenye Hoteli ya
Sea Cliff, Dar es Salaam, washtakiwa hao waliomba rushwa ya sh. milioni 10 kutoka kwa Bw. Wage.

Ilidaiwa kuwa, washitakiwa hao waliomba rushwa ili kuzuia habari inayoelezea tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma inayomuhusu Bw. Wage akiwa Mhasibu wa halmashauri hiyo isirushwe katika televisheni ya TBC1.

Bw. Muro alikamatwa Januari 31,2011 baada kwa tuhuma hizo na kushikiliwa kwa saa saba kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Kati, Dar es salaam na baadaye kuachiwa.

Washtakiwa hao walifikishwa mahamani na kusomewa mashitaka yao na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Bw. Boniface Stanslaus, akisaidiana na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Bw.
Ben Lincolin, mbele ya Hakimu Mkazi, Bw. Gabriel Mirumbe.

Baadaye washtakiwa wote waliachiwa kwa dhamana baada ya kusaini hati ya dhamana ya sh. milioni tano kila mmoja na kuwa
na wadhamini wawili wa kuaminika hivyo kuendelea kufika mahakamani wakati kesi ikiendelea.

Juni 2011, upelelezi wa kesi hiyo ulikamilika ambapo upande wa mashitaka ulidai utakuwa na mashahidi 11, wakati Bw. Wage akiwa mmoja wa mashahidi hao.

No comments:

Post a Comment