21 November 2012

Wahukumiwa miaka 15 kwa kuingia hifadhini bila kibali


Na Mwandishi Wetu, Babati

MAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, imewahukumu wakulima watatu kwenda jela miaka 15
na kulipa sh. milioni mbili kila mmoja wakimaliza kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya kuingia katika Hifadhi ya Taifa
ya Tarangire bila kibali.

Mbali ya kupatikana na kosa la kuingia hifadhini bila kibali, washtakiwa hao pia walipatikana na hatia ya kuingia katika
hifadhi hiyo wakiwa na bunduki moja aina ya riffle, risasi 19
na silaha za jadi kama shoka, sime na vyakula mbalimbali.

Washtakiwa hao ni Habibu Ally, Shabani Hamisi wate wakazi wa Kijiji cha Emboreet na Esrael Lukumay, mkazi wa Kijiji cha Terati, Wilaya ya Simanjiro, mkoani humo.

Hakimu wa Mahakama hiyo Bw. Victor Bigambo, alissema Mahakama hiyo imeridhika na ushahidi uliotolewa na Jamhuri
ambapo adhabu iliyotolewa ni fundisho kwa wengine.

“Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa dhidi ya watuhumiwa na kuwatia hatiani hivyo watatumikia kifungo cha miaka 15 gerezani kila mmoja na kulipa sh. milioni 2 kila mmoja baada ya kutoka jela, hii itakuwa fundisho kwa wote wenye tabia kama hii,” alisema.


Awali Mwendesha Mashtaka wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Bw. Linus Bigamwa, aliiomba Mahakama hiyo
kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa kwani vitendo vya kuingia hifadhini na silaha, matukio ya ujangili yanayoongezeka mara kwa mara licha ya kuwepo kwa sheria lakini zimekuwa zikipuuzwa.

Katika utetezi wao, washtakiwa hao waliieleza Mahakama kuwa waliingia hifadhini ili kutafuta mifugo yao iliyokuwa imepotea  ambapo utetezi huo haukusaidia kuwanasua na adhabu hiyo.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani humo, linawashikiliwa wakulima wawili Emmanuel Feo (41) mkazi wa Kijiji cha Boay
na Hassani Salimu (40) mkazi wa Galapo, kwa tuhuma za kukutwa na vipande vinne vya pembe za ndovu zenye thamani ya sh. milioni 23.7 kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa mkoani humo, Akili Mpwapwa, aliyasema hayo juzi na kudai kukakatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya jeshi hilo, askari
wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na wasamaria ambao wamekuwa wakitoa mchango mkubwa ili kukomesha vitendo vya ujangili.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku baada ya kupata taarifa za watuhumiwa kutaka kuuza vipande vinne vya pembe hizo, hivyo kwa kushirikiana na askari wa hifadhgi  waliweka mtengo uliofanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao.

“Matukio haya yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo hayo, lakini tumejipanga kuhakikisha tunayakomesha na sina shaka yatakoma, tunachoomba wasamaria wema waendelee kutupa taarifa za uhalifu huu,” alisema Kamanda Mpwapwa.

Aliongeza kuwa, upepeleza wa tukio hilo unaendelea na baada ya kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

No comments:

Post a Comment