26 November 2012

Vigogo BoT walipa faini kukwepa kifungo



Na Rehema Mohamed

MAOFISA watatu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao juzi walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh. milioni 5 kila mmoja, jana wameachiwa huru baada ya kutimiza sharti la kulipa kiasi hicho cha fedha.


Hukumu hiyo ilitolewa Jopo la Mahakimu watatu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Bw. Samuel Kalua, Bw. Ilvin Mugeta na Bi. Beatrice Mutungu.

Maofisa hao ni Bi. Ester Komu, Bi. Sophia Kalika, Bw. Immani Mwakosya ambapo ndugu zao walionekana mahakamani hapo wakifanikisha taratibu za kulipa faini ili waende gerezani
kuwatoa ndugu zao.

Kesi iliyokuwa ikiwakabili Maofisa hao ni wizi na kuisababishia BoT hasara ya zaidi ya sh. bilioni 3.8 zilizoibwa kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Katika kesi hiyo, Maofisa hao walitiwa hatiani na kosa la uzembe kazini wakiwa wanatekeleza majukumu yao katika benki hiyo.

Maofisa hao walihusishwa na kesi hiyo baada ya kudanganya kuwa, Kampuni ya Mibare Farm, imepewa deni na Kampuni ya Textile Mills Ltd ya India na kujipatia ingizo la zaidi ya sh. bilioni 3.8.

Hata hivyo Bi. Komu ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Madeni BoT, bado anaendelea kuhusishwa na kesi ya EPA ambayo inaendelea kusikilizwa na Mahakama hiyo.

Kesi hiyo ni ile ya kuisababishia BoT hasara ya sh. bilioni 5.9,
baada ya kudanganya kuwa, Kampuni ya Liquidity ilipewa deni
na kampuni ya M/s Societe Alsacienne De Cconstruction De Machines Taxtiles ya Ufaransa wakati si ukweli.

No comments:

Post a Comment