26 November 2012

Umakini wa Zitto tumaini la Taifa


Na Gladness Mboma

BWANA Zitto Kambwe Mbunge wa Kigoma Kaskazini ni Mwanasiasa aliyechipukia katika duru ya siasa nchini, kwa kutoa hoja zenye ukweli na serikali kulazimika kuzifanyia kazi,hali hiyo imesababisha aonekane kwamba anafaa katika uongozi wa juu kutokana na kutoa kauli nzito zenye kusaidia Watanzania.

Asimamapo Bw. Zitto iwe bungeni au mkutanoni kila mtu ukaa vizuri kumsikiliza kutokana kauli zake zenye ukweli,ambapo uungwa mkono na watu wengi wakiwemo wanasiasa wenzake.

Bw.Zitto ni mwanasiasa ambaye pamoja na kukosolewa kutokana na hoja zake zenye ukweli hata siku moja utamuona akikasirika au kuja juu (kuhamaki)kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wenzake wasiopenda kukosolewam wanapokosolewa uhamaki.

Wiki hii, Bw. Zitto Kabwe ni mtu wa pili kuhojiwa katika mjadala ulioongozwa na Asha Dii kwa niaba ya wanachama wa JamiiForums, ambapo wanajamii walipata fursa ya kumhoji mambo mbalimbali yatokanayo na siasa, ambapo alijibu mjadala wote kwa kujiamini.

Kwanza kabisa Bw. Zitto alianza kujibu kwa kueleza historia fupi ya maisha yake, ambapo alisema kwamba yeye ni Mtanzania aliyezaliwa Kigoma, Kijiji cha Mwandiga na kukulia katika kitongoji cha Mwanga.

Shule ya msingi alisoma Kigoma na shule za sekondari alizosoma ni pamoja na Kigoma, Kibohehe Moshi, Galanos Tanga na Tosamaganga Iringa.

Elimu yake ya juu ameipata katika Chuo Kikuu cha Zanzibar kwa mwaka mmoja, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Uchumi, na kusomea masuala ya biasha nje ya nchi, Biashara ya kimataifa na shule ya sheria,uchumi wa biashara ya madini.

Bw.Zitto ni mwenyeji wa Kijiji cha Kibingo, Kata ya Mwandiga Wilaya ya Kigoma kwa hapa Dar es Salaam anaishi maeneo ya Tabata,akiwa mjini Dodoma nyakati za bunge uishi na Mama yake mzazi pamoja na wadogo zake.

SWALI:Unalizungumziaje Ombwe la Itikadi miongoni mwa vyama vyetu vya Siasa, ambapo tangia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaingie nchini?

JIBU: Ni vigumu kutofautisha itikadi za vyama vya siasa kinadharia na kivitendo hasa ukizingitia ukweli kwamba,kila chama sera na itikadi zinazouzwa au kutekelezwa ni za kiliberali, huku wananchi wengi hasa vijijini wakiwa hawana ufahamu juu ya madhara na faida ya itikadi hii ni nini.

Hii ni changamoto kubwa sana kwa nchi yetu.Itikadi za kisiasa husaidia kunyoosha sera za vyama, hivi sasa chama chochote kinaweza kuwa na sera yeyote ile kwa kuwa hakuna uti wa mgongo ambao ni itikadi.

Lazima vyama vijipambanue kwa itikadi zao, kwani kwa kukosekana kwa itikadi zinazoeleweka vyama vimekuwa kama 'electoral machines' tu. Kukosekana kwa itikadi kunafanya vyama kudandia masuala.Mfano juzi hapa mmesikia Mkutano Mkuu wa CCM umeazimia elimu iwe bure.

"CHADEMA tulisema hivyo mwaka 2010, CCM wakasema huo ni uwendawazimu, kwani haiwezekani. Nakumbuka nilikuwa kwenye mdahalo pale Serena mwaka 2010, vijana wa CCM wakaniuliza mtapata wapi pesa za kusomesha watu bure

"Nikawajibu kama tuliweza kuwasomesha bure kwa Tumbaku, Kahawa na Pamba, tutawasomesha bure kwa dhahabu, tanzanite. Leo CCM wanasema elimu bure. Nimemsikia Lowassa juzi anasema inawezekana. Lowassa huyu nilibishana naye sana mwaka 2010 akisema haiwezekani. Huu ni ukosefu wa itikadi sahihi,"anasema.

Viongozi hawasomi, hivyo bongo zao hazipo 'sharp' kuweza kuona ni mwelekeo gani wa itikadi wa kufuata. At best tunaimba kama kasuku itikadi zilizoendelezwa nje, hakuna ualisia.

SWALI:Unaiongeleaje sera ya Majimbo ya CHADEMA?”

JIBU:Ni utekelezaji wa kushusha madaraka mikoani,kupanua uwajibikaji na kuleta maendeleo kwa wananchi. Sera hii ya utawala ndio suluhisho la masuala mengi ya uwajibikaji hapa nchini.

Kuna haja ya kuwa na DC? Kwa nini wakuu wa mikoa wasichaguliwe na wananchi? Tulipoamua kupendekeza sera hii kwa wananchi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 tuliambiwa sisi tuna lengo la kuleta ukabila nchini.

Inawezekana kuna maeneo fulani fulani tulikosea mkakati. Kwa mfano tulianza kusemea suala hili tukiwa mkoani Kilimanjaro kwa hiyo CCM ikadakia 'unaona wachaga hawa' sasa wanataka nchi kwao. Kimkakati tulikosea.

Anasema walipaswa kuzindua sera hii kanda ya Ziwa au kanda ya Kusini. Tulijifunza kutokana na makosa haya. Hivi tumejiandaa vizuri zaidi kuielezea sera hii. Tunataka kuimarisha Halmashauri za Wilaya,Miji,Manispaa,Majiji kwa kuoondoa nafasi ya Wakuu wa Wilaya na kada nzima pale Wilayani.

"Majukumu yote ya kisiasa ya DC atayafanya Mwenyekiti wa Halmashauri. Majukumu yote ya Kiutendaji ya Ofisi ya DC atayafanya Mkurugenzi wa Halmashauri

"Wakuu wa mikoa wachaguliwe na Wananchi moja kwa moja na wawe na 'executive powers' kwa mambo ya mkoa husika. Tutayaweka kisheria mambo haya. Hii mambo ya Rais kuteua wakuu wa Mikoa nchi nzima hapana. Watu wachaguliwe,"anasema.

Anasema kuwa anaamini kabisa kuwa Sera hiyo ikitekelezwa wanaweza kutumia rasilimali vizuri na mikoa itashindana kimaendeleo badala ya kushindana kwa namna walivyompokea Rais mkoani kwao.

SWALI:Unaona tofauti ya msingi kati ya CCM na CHADEMA ni ipi?

JIBU:CCM imeshindwa kupambana na adui ufisadi, CHADEMA tunapambana na tutapambana na ufisadi kwa nguvu zetu zote. CCM inaamini katika soko holela, CHADEMA tunaamini katika soko linalojali.

Anasema CHADEMA inaamini katika nguvu ya Umma, CCM inaamini katika nguvu ya Dola.

SWALI:Nini kinakuvutia ndani ya CCM ambacho hakipo CHADEMA?

JIBU:Sijakiona bado

SWALI: Bado unafikiri wewe kuwa CHADEMA ni tija kwa jamii kuliko kuwa Chama kingine mfano CCM?

JIBU:Jamii imefaidika sana kuwa kwangu CHADEMA.

Anasema kupitia bunge na nje ya bunge ameweza kuisimamia Serikali kwenye mengi na hasa masuala ya rasilimali za Taifa kama madini na kufanikiwa kupata sheria mpya ambayo imetoa fursa kwa Watanzania kufaidika na utajiri wao wa madini.

Mengi sana ninayofanya nikiwa CHADEMA nisingethubu kuyafanya ningalikuwa CCM.

SWALI:Unalizungumziaje suala la kuwa na utitiri wa vyama vingi vya siasa vinavyokula pesa za walipa kodi halafu havina tija wala mchango wowote kijamii zaidi ya kutufilisi.Je kuna umuhimu wa kuifanyia sheria mabadiliko ili kuwe na ukomo mfano, vyama vitatu tu?

JIBU:Ndio Demokrasia.

Tusiminye kabisa watu kuwa huru kuanzisha vyama vya siasa. Baada ya muda ni vyama vyenye uwezo wa kukonga nyoyo za wananchi ndio vitabakia. Wala hatuna haja ya kuweka sheria.

Huko mbele ninaona Tanzania yenye vyama sio zaidi ya vinne.Vyama vikubwa viwili, CCM na CHADEMA. na CUF watakuwa balancing party kama ilivyo LibDems UK au Greens and Liberals Ujerumani.

Kwa hali ya sasa ya muungano ninaona kuwa CUF yaweza kuwa kama The Bloc Québécois ya kule Canada. sioni NCCR ikidumu. Sioni future ya UDP bila Cheyo na TLP bila Mrema.

Lakini pia kuna uwezekano mkubwa sana wa kundi moja la CCM kuunda chama kingine cha siasa ambacho kinaweza kuwa na nguvu hata zaidi ya CHADEMA. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 tutaona hivi new configurations. Tuache watu wawe huru kuunda vyama. Vyenye nguvu vitabakia

SWALI:Nini kipaumbele chako cha sasa kama    mwanachama wa CHADEMA?

JIBU:Kutumikia chama changu kwa nafasi nilizonazo.

Natumia nafasi yangu ya Ubunge na Uwaziri kivuli kuhakikisha kuwa chama kinapata taswira chanya mbele ya jamii, Na kinaleta mabadiliko ambayo chama tawala, yaani CCM, kinashindwa kuwafikishia wananchi.

Utaona kwamba, kama unafuatilia Bunge, hakuna mkutano wa Bunge unaopita bila hoja mahususi inayojenga taswira chanya ya chama.

Ni bahati mbaya sana kuwa hatutumii baadhi ya mafanikio yetu Bungeni kwenye ulingo wa siasa na hivyo kuwaacha CCM wanachukua credits.

Kwa mfano ni kwanini mafanikio ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu hatujayafanyia kazi ya kisiasa? Ingawa hatukufanikiwa kumtoa Waziri Mkuu, lakini tuliilazimisha Serikali kufanya mabadiliko.

"Rais Jakaya Kikwete  alisema ni upepo tu, lakini upepo huu ulikuwa na joto kali ukamshinda na tukaacha yeye achukue 'credit' kwa kazi yetu ya uwajibikaji

"Hoja ya juzi ya Bi.Halima Mdee kuhusu ardhi inabidi kuifanya ni ajenda ya kisiasa. Hoja ya Mkonge tulikwenda Tanga na ilikuwa na mafanikio makubwa sana. Hoja ya Mabilioni ya Uswiss nayo tunaiachia wanaisemea watu wa CCM kuififiza,"anasema.

Historia inatuonyesha kuwa hoja zote tulizozitumia vizuri nje ya Bunge zilijenga taswira nzuri ya chama kuanzia Buzwagi na EPA.

SWALI:Mkuu ni kweli kuwa CHADEMA ni chama cha kidini,kikabila? Na kama ni kweli, tatizo hilo lishughulikiwe vipi? Kama si kweli, unaweza kuueleza umma wa Watanzania una kauli gani juu ya mitizamo hii dhidi ya chama chenu?

JIBU: CHADEMA ni chama cha kitaifa. Kingekuwa chama cha kidini au kikabila kingefutwa. Katika uongozi wa Chadema unapata watu toka mikoa na kabila mbali mbali, pia watu toka dini mbali mbali. Aina mbalimbali hii haipatikani katika vyama vingi humu nchini.

Nadhani mtazamo huu unapandikizwa na watu ambao hawakipendi chama chetu na wanaona chama kama tishio kwa maslahi yao binafsi.

Pia sisi kama chama tunapaswa kuwa makini sana, hasa viongozi tunapofanya kazi zetu ili kutothibitisha taswira hii mbaya dhidi ya chama chetu. Baadhi ya wanachama wa CHADEMA ndio mabingwa wa kueneza jambo hili.

CCM nao humo humo wanapandikiza mbegu za chuki. Unakuta Waziri wa CCM anamwita Mbunge wa CHADEMA na kumwambia, fulani bwana mdini sana. Mwangalieni.

Kiongozi wa CHADEMA anajiona kapata bonge ya issue na kueneza. Tunachinjwa na CCM kwa upuuzi wetu. Kwa ujinga wetu wenyewe. Chama chetu kimesambaa nchi nzima na viongozi wake ni wa dini zote na makabila yote.

SWALI:Unaizungumziaje demokrasia ndani ya chama chako katika chaguzi teuzi na kupanga safu za uongozi?

JIBU:CHADEMA ina demokrasia ya aina yake na wanachama tunaridhika nayo. Chama kinatekeleza matakwa yenu au kisitekeleze na kila mwanachama lazima atii utekelezaji huo wa haki. Tuna utaratibu mzuri sana wa kujieleza na kutetea hoja zetu ndani ya chama.

Na baada ya watu wote kukubaliana tuna hakikisha tunasimama wote kwa kauli moja sehemu zote tunapo wakilisha chama. Sio katika kupanga safu za uongozi tu, ni sehemu zote za uongozi wa chama.

SWALI:Kwanini CHADEMA haiwatumii viongozi wa Mikoa na Wilaya na badala yake inatuma watu toka makao makuu hata kwa mambo madogo madogo ambayo yangemalizwa na uongozi wa ngazi husika?

JIBU:Huo mtazamo unaweza kutokana na kulinganisha Chadema na vyama vingine. Ieleweke kuwa Chadema ni chama tofauti na kina utaratibu wake. Katika chama chetu Viongozi wa mikoa na wa wilaya wana majukumu yao na makao makuu pia wana majukumu yake.

Inaweza kutokea mara kwa mara hizi hatua mbili zishirikiane katika kutekeleza kazi za chama. Hata hivyo, tunaendelea kujenga chama kama taasisi, na pia tunaendelea kujenga uwezo wa viongozi wetu wa mikoa na wilaya ili waweze kumudu majukumu mengi zaidi na kuwaachia wenye kukaa makao makuu kuhusika zaidi na 'strategies' za chama.

SWALI:Unazizungumziaje harakati za M4C na athari  yake kisiasa na kijamii? Chama kimeweka taratibu gani nzuri za malezi kwa wanachama wapya wanaojiunga kwenye M4C, kama bado huku si kusuka kamba inayoungua?

JIBU:Kwa sababu jina lake liko wazi kabisa, M4C ni moja ya operesheni inayo fanikisha Watanzania kujiunga katika chama huku wakijua kabisa kuwa malengo ni kuleta mabadiliko chanya.

Athari yake kwa jamii ni kubwa sababu inawaweka wanachama wenyewe kuwa vyanzo vya mabadiliko. Baada ya kujiunga, ni obvious kuwa Chama kinatoa mafunzo kwa wanachama wake wapya na hivyo kuwalea kuwa makada wazuri. Hii sio operesheni ya kwanza ya Chama na haitakua ya mwisho.

M4C sio chama ndani ya chama, M4C ni operesheni ya kujenga chama na kuleta mabadiliko nchini.

Inaendelea jumapili ijayo    
 

         

No comments:

Post a Comment