26 November 2012

Hifadhi ya Saanane kivutio cha watalii ndani na nje


Na Jovin Mihambi

MOJAWAPO ya shughuli za serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ni kuendeleza sekta ya utalii wa ndani na nje ili kuweza kuliongezea Taifa pato kubwa linalotokana na sekta ya utalii.


Kutokana na hilo, sekta ya utalii kuundiwa chombo ambacho kinaratibu shughuli za utalii nchini, ambacho kiko chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambalo ni Shirika pekee ambalo limeundwa na serikali katika kusimamia shughuli hizo.

Kisiwa cha Saanane ambacho kiko katika Ziwa Victoria nje kidogo ya jiji la Mwanza, kina historia kubwa ambayo inaongezea umaarufu wake. Umaarufu wa kwanza ni kwamba kisiwa hicho ni kidogo kuliko visiwa vyote nchini pamoja na kuwa ni kisiwa chenye vivutio vikubwa na kuwa karibu na jiji la Mwanza.

Umaarufu wake mwingine ni kwamba ni hifadhi ya pili katika Ziwa Victoria ambalo ni ziwa la pili kwa ukubwa Duniani pia lenye maji baridi, hifadhi pekee Tanzania yenye ‘De Brazas Monkey’ (Tumbili weusi) pamoja na kuwa ni eneo wakilishi lililohifadhiwa kisheria lenye kumbu kumbu ya mazingira asilia ya Jiji la Mwanza.

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane ipo Kusini Magharibi ya jiji la Mwanza katika wilaya ya Nyamagana. Awali ilikuwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 0.76 ikijumuisha eneo la nchi kavu na maji kwa mzunguko wa mita 100 kutoka ufukweni.

Hivi sasa hifadhi hiyo inao ukubwa wa kilomita za mraba 2.18 kwa kujumuisha kwa Kisiwa cha Saanane chenye ukubwa wa kilomita za mraba 0.76 na visiwa vya Chankende Kubwa na Chankende Ndogo vyenye ukubwa wa kilomita za mraba 0.1 na eneo la maji linalozunguka visiwa hivyo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1.32

Mwaka 2006, Serikali ilitanga azma yake ya kupandisha hadhi ya Uhifadhi wa eneo hilo kuwa Hifadhi ya Taifa chinii ya usimamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo Oktoba, mwaka huu lilipitisha kisiwa hicho kuwa Hifadhi ya Taifa.

Bi Bayona anavitaja vivutio vinavyopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Saanane ni pamoja na wanyamapori asilia na wale ambao wamepandikizwa ikiwemo pimbi, fisi maji, paka mwitu, mamba, mijusi na aina mbali mbali ya samaki aina ya sato, sangara na samaki wengine. Kuna pia nyoka mbali mbali pamoja na chatu, ndege aina mbali mbali wa aina mbali mbali zaidi ya sabini wanaojumuisha wahamiaji na wakazi (migratory and resident birds).

“Pia kuna baadhi ya wanyama ambao wamepandikizwa kama vile swalapala, tumbili, kobe ‘De-brazas Monkey’ ambao ni jamii ya tumbili weusi ambao wanapatikana pekee katika nchi ya Tanzania.

Mhifadhi Mkuu wa Kisiwa cha Saanane Bi. Haika Bayona anatoa historia fupi ya kisiwa hicho kwamba chimbuko la jina la Saanane ni kutokana na mkazi wa awali na pekee katika kisiwa hicho ambaye alikuwa akiishi kisiwani humo alikuwa akijulikana kwa jina la Saanane Chawandi ambaye aliishi kisiwani humo.

Alikuwa akiishi pamoja na familia yake huku akijishughulisha na shughuli za kilimo na ufugaji. Baadaye serikali kwa kutambua umuhimu wa kisiwa hicho, ilimuhamishia katika kisiwa jirani baada ya kumlipa fidia ili kupisha shughuli za uhifadhi.

Anasema kuwa uhifadhi wa eneo hilo ulianza rasmi kisheria mwaka 1964 ikiwa ni Bustani ya kwanza ya wanyamapori (zoo) nchini na kusimamiwa na serikali kupitia Halmashauri ya Mkoa wa Mwanza ambayo ilipewa majukumu ya kusimamia shughuli za kisiwa hicho.

Lengo la kuhifadhi bustani hiyo lilikuwa ni kutoa elimu ya uhifadhi na burudani ya utalii kwa wakazi na wageni ambao walitembelea Mwanza. Na mwaka 1991 Saanane ilitangazwa kuwa Pori la Akiba kwa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 12 ya mwaka 1974.

Anasemaa kuwa kisiwa cha Saanane pia kilitumiwa na shirika la Ujerumani la ‘Frankfurt Zoological Society’ kama makazi ya muda kwa ajili ya kuzoesha wanyama waliopandikizwa katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo kilichoko mkoani Geita.

Kuhusiana na shughuli za utalii, Bi Bayona anasema kuwa tangu mwaka 2008 hadi Oktoba, mwaka huu, jumla ya wageni waliotembelea hifadhi hiyo kutoka nchi za nje ni 632 na wageni kutoka ndani ya nchi ni 15,488 na kufanya jumla ya wageni ambao wametembelea hifadhi hiyo kufikia 16,120 na kuingiza mapato ya serikali kiasi cha shillingi 85,534,121.

Hifadhi imeanza kukusanya mapato yake baada ya Idara ya Wanyamapori kuondolewa majukumu hayo ya ukusanyaji wa mapato. Hifadhi hadi sasa inapokea wastani wa wageni wa ndani 232 na wageni wa nje 14 kwa mwezi.

Mwaka 2009/2010 mhifadhi huyo mkuu anasema kuwa mapato yaliongezeka kutokana na hifadhi kutumia boti zake na tozo mpya kwa wageni na kusema kuwa wageni wa ndani wakubwa hulipa sh.2,000 na watoto sh.1,000 ambapo wageni wa nje hutozwa dola za kimarekani 30 kwa wakubwa na watoto dola 15.

Lakini anasema kuwa kuanzia mwaka 2010/2012 wageni wamepungua kutokana na hifadh kukosa usafiri wa boti kwa muda wa miezi mitatu.

Mkuu wa Hifadhi, Bi Bayona anasema kuwa baadhi ya Bunge kupitisha hifadhi hiyo kuwa ya taifa, anayo mikakati kabambe ya kuweza kuboresha hifadhi hiyo baada ya kufanyia tafiti mbali mbali ambao anasema kuwa umefikia hatua ya kukamilika zikiwemo wa kufahamu hali ya rutuba ya udongo ili kufahamu uwezo wa Hifadhi kustahimili ukuaji wa malisho ya wanyamapori, utafiti wa kutambua idadi ya wanyamapori wanaoweza kuhifadhiwa katika hifadhi (Ecological Carrying Capacity) umekamilika.

Utafiti mwingine ambao tayari umekamilika ni wa upandikizaji wa wanyamapori ambao anasema kuwa umekamilika unaowezesha hifadhi kutambua wanyamapori wanaoweza kupandikizwa, tathmini ya mazingira (EIA) pamoja na uandaaji wa orodha ya ndege ambao ni muhimu kwa ajili ya utalii.

Kazi ambazo kwa sasa zinaendelea ni kuondoa mimea isiyo asili na baadhi ya mabanda ya zamani (wild cages) ili kuruhusu uoto asili pamoja na ufuatiliaji wa afya za wanyamapori na udhibiti wa magonjwa ya wanyama.

Anasema pia, mbali na tafiti hizo, hifadhi ipo katika hatua za kuongeza wanyamapori kwa awamu ya kwanza mwaka huu wa fedha 2012/13 baada ya kukamilika kwa tathmini (EIA), taratibu za ununuzi wa boti zinaendelea ili kununua boti mwaka huu wa fedha 2012/13 pamoja na kuendelea kujitangaza ndani na nje ya nchi.

Bi Bayona anabainisha kuwa mbali na shughuli zingine, kuna mafanikio yamepatikana katika utendaji kati katika hifadhi ya Saanane ambayo ni pamoja na kufanyika kwa baadhi ya tafiti muhimu kiikolojia nne, uwepo na Rasmu ya Mpango wa Uendeshaji wa Hifadhi, ujangili kuendelea kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa pamoja na ununuzi wa baadhi ya vitendea kazi muhimu ikiwemo gari moja, silaha, boti mbili na injini pamoja na pikipiki mbili, ununuzi wa viwanja sita vya makazi ya watumishi na ujenz wa nyumba za watumishi.

Mafanikio mengine ni ujenzi wa ukarabati wa baadhi ya miondombinu ya utawala na utalii pamoja na tukio ambalo ni muhimu katika historia ya hifadhi nchini la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane ambapo mshiriki mkuu katika mchakato huo ni Mhifadhi Mkuu wa Saanane wa sasa.

Anasema kuwa shughuli za utafiti ili kuboresha hifadhi hiyo zinaendelea kadri bajeti inavyotengwa na pia hifadhi inaendelea kushirikiana na Taasisi mbali mbali za utafiti kama vile Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori na Rasilimali za samaki, Vyuo Vikuu na watafiti binafsi.

Kuwepo wa Kisiwa cha Saanane ambacho ni hifadhi ya taifa ni fursa kubwa ya kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana mkoani Mwanza, Kanda ya ziwa pamoja na hifadhi zingine za taifa hivyo kukuza pato la shirika la TANAPA na jamii kwa ujumla. Na kuna kila dalili ya kumpongeza Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saanane, Bi. Bayona kutokana na kupandisha kisiwa hicho hadhi dalili ambazo zinaonyesha kwamba wanawake wanaweza hata bila kuwezeshwa.







No comments:

Post a Comment