26 November 2012

Alichonena Lowassa kinapaswa kufanyiwa kazi


Na Michael Sarungi

KATIKATI ya wiki iliyopita Waziri Mkuu aliyejiuzulu.Bw. Edward Lowasa,alitoa alitoa wito kwa serikali akisema kuwa huu ni wakati muafaka kwa elimu ya sekondari kutolewa bure kama ilivyo elimu ya msingi.

Waziri mkuu huyo wa zamani alitoa kauli hiyo wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati.

Katika harambee hiyo,Bw. Lowasa alisema serikali inapaswa kugharamia elimu ya sekondari bila ya woga na mwananchi anapaswa kuchangia mahitaji mengine kidogo kwa kile alichodai ni kwamba wakati huu kila Mtanzania anapaswa kuwa na elimu ya sekondari.

Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuunga mkono wito uliotolewa na Rais Kikwete wa kutaka kila shule ya sekondari kujenga maabara pamoja na lile la elimu ya sekondari sasa kuwa ni elimu ya lazima kwa kila mtoto na itolewe bure.

Namnukuu, Bw.Lowassa,“Elimu ya sekondari itolewe bure kama tunavyo fanya kwenye  elimu ya msingi, watoto wasome bure kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne wadau mbali mbali wawe mstari wa mbele kuchangia masuala ya elimu ili siku za baadaye vijana waweze kujikwamua”.

Hili ni wazo ambalo kwa miaka mingi limekuwa likipigiwa kelele na Watanzania wengi hususani wenye uchungu na kizazi kijacho.

Watanzania hao wamekuwa wakisema kuwa Taifa lisilo kuwa na elimu ni sawa na mfu.

Hakika hili ni wazo zuri kuwahi kutolewa na hawa viongozi wetu tulionao katika siku za hivi karibuni, kwani ni wazo ambalo endapo litapokelewa na wahusika na kufanyiwa kazi linalenga kuwakomboa watoto wengi wa walala hoi wanaoshindwa kuipata elimu ya sekondari kutokana na matatizo ya kiuchumi.

Ni wazi kuwa hakuna Mtanzania asiyefahamu ugumu wa maisha unao wakabili Watanzania walio wengi  hususani wanaoishi maeneo ya vijijini ambako ndiko waliko Watanzania wengi na ambao wanaishi kwenye lindi kubwa la umaskini.

Kama alivyosema,Bw. Lowassa huu ni wakati kwa kila Mtanzania mpenda haki kuanza kupaza sauti yake kwa kushiriki kwa hali na mali ili kuhakikisha kuwa elimu hii ya sekondari inaanza kutolewa bure lengo likiwa ni kuhakikisha elimu inawafikia hata Watanzania maskini.

Tuanze kuipigia makelele serikali ili ikisikie kilio hiki cha watoto wa hawa maskini wa Kitanzania wanoishia darasa la saba kila mwaka kwa kukosa ada za kuwapeleka shule.

Ikumbukwe kuwa Bw. Lowasa siyo mtu wa kwanza kuitaka serikali kuhakikisha elimu ya sekondari ianze kutolewa bure hata Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Dkt.Willbrod Slaa katika kampeni zake za kugombea urais aliwahi kuieleza serikali kuhusu jambo hilo.

Kwa vilio hivyo nashawishika kuileza serikali  isitake kuendelea kuishi kwa kutegemea ngojera zake za kila siku za kuwa haina pesa huku kila kukicha tunashuhudia matumizi ya anasa yasiyo kuwa na tija kwa mwananchi wa kawaida.

Matumizi kama kupandishiana mishahara mara dufu, kutumia mabilioni ya shilingi kwenye chaguzi za ajabu ajabu, matumizi ya mabilioni kwenye sherehe za uhuru wakati shuleni hakuna madawati,shuleni hakuna vitendea kazi na hii  ni mifano michache tu ya matumizi mabaya.

Ifike wakati sasa kwa viongozi wa serikali waone aibu kwa vitendo wanavyovifanya kwa kujilimbikizia mali huku wananchi wakiendelea kukamuliwa kodi ambazo hazina maslahi kwao.

Nasema hivyo kutokana  na mifano iliyo hai ambapo tunashuhudia matumizi mengi kama nilivyosema hapo awali  huku watoto wetu wakipata tabu ya kupata elimu inayostahili.

Mwisho namalizia kwa  kuishauri serikali kuachna na mzaha huu kwani kama itaendelea  kufanya  hivyo taifa ili litaendelea kuzalisha  mambumbu

No comments:

Post a Comment