19 November 2012

Tume ya utumishi wa mahakama tuhuma dhidi yenu hamjazijibu


NA Michael Sarungi.

KATIKA siku za hivi karibuni vyombo mbali mbali vya habari viliripoti kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama imemjia juu Mbunge wa Singida Mashariki,Bw.Tundu Lissu, kuhusu kauli yake ya kuwapo upungufu katika uteuzi wa majaji hapa nchini.

Katika ripoti yake hiyo, tume hiyo inasema kuwa hakuna jaji hata mmoja mwenye upungufu wa sifa za kuwa jaji au aliyeteuliwa na mamlaka ya uteuzi bila ya kupendekezwa na chombo husika.

Huo ni utetezi uliotolewa na Katibu wa tume hiyo, Bw Hussein Katanga, kwenye vyombo vya habari kujibu tuhuma zilizotolewa na msemaji wa kambi  rasmi ya upinzani bungeni wa Wizara ya Katiba na sheria.

Labda nianze kwa kumuuliza,Bw.Katanga kuwa kwa mwananchi wa kawaida anaweza kumwamini nani kati yake na huyo msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa kuzioanisha taarifa  yake hiyo na utetezi wa Bw. Lissu?

Katika ushahidi wake mzito aliopata kuutoa mbele ya Kamati ya Haki na  Maadili, mbunge huyo anakwenda mbali kwa kuonesha takwimu namna gani kwa nyakati tofauti marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamewahi kuvunja katiba ya nchi.

Bw.Lissu anasema kwamba marais hao walivunja Katiba ya nchi kwa kuwaongezea muda na kuwateua majaji waliofikisha muda wa kustaafu kwa mujibu wa sheria tuhuma ambazo hazijapata ufafanuzi wa kina mpaka leo hii.

Katika orodha yake hiyo, Bw.Lissu, alifikia hatua hata ya kuwataja kwa majina majaji wasio kuwa na sifa ya kuwa majaji katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa akiwemo mmoja aliyelazimishwa kuingia darasani Chuo Kikuu Huria (OUT),ili apate shahada ya sheria kwa mujibu wa sheria.

Msemaji huyo wa masuala ya Katiba na Sheria Bungeni hakuishia hapo kwani katika utetezi wake huo alienda mbali na kusema kuwa majaji wengine waliteuliwa kushika nafasi hizo nyeti huku wakikabiliwa na tuhuma za rushwa na ukiukaji wa maadili ya kazi wakiwa mahakimu na wanasheria.

Aidha aliwataja majaji wasio kuwa na uwezo wa kuandika hukumu akitolea mfano wa jaji mmoja aliyepata kushindwa kuifanya kazi hiyo kwa kipindi cha miaka minne kisha kunyang’anywa na aliyekabidhiwa na akaifanya kwa wiki nne tu.

Katika utetezi wake huo,Bw.Lissu, aliwataja majaji wengine mbao ni wagonjwa na ambao tangu wateuliwe hawajawahi kusikiliza kesi na kuzitolewa hukumu.

Katika utetezi huo mrefu, msemaji huyo alitaja vitu vingi ambavyo vimekuwa vikifanywa na wahusika kuwateua majaji kitu ambacho ni hatari sana kwa mstakabali wa taifa.

Akamalizia utetezi wake kwa kusema kuwa hapa nchini sasa hivi watu wanateuliwa kuwa majaji wa Mahakama Kuu ambao hata hawajawahi kupendekezwa na tume ya utumishi wa mahakama kwa sababu hiyo hawajawahi kufanyiwa upekuzi (Vetting)
wowote na mamlaka husika ya kikatiba.

Utetezi huu wa msemaji wa kambi rasmi ya bunge katika masuala ya katiba na sheria ulitolewa hapa, baada ya kambi hiyo kuwasilisha maoni yake kuhusu mpango na mabadiliko ya matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha ya mwaka 2012/13.

Ikumbukwe kuwa maoni hayo ya kambi rasmi yalizua mjadala mkubwa ndani ya idara hiyo mpaka ndani kiasi cha wachangiaji wengi wakimtuhumu msemaji huyo wa kambi kuwa ameidhalilisha mahakama.

Aidha msemaji huyo alishambuliwa kwa kudaiwa kuwa ni mfitini na asiye kuwa na akili hata kidogo na ni mtu ambaye ni hatari kwa mstakabali wa ustawi wa taifa hili.

Sasa kulingana na umuhimu na unyeti wa mamlaka husika tungetarajia wahusika kuja na utetezi wa dhati juu ya tuhuma hizo kuliko wahusika kuja na propaganda za kisiasa ambazo hazina tija yoyote kwa Watanzania.

Idara hii ya mahakama ni nyeti na ni muhimu kwa masuala yote  ya utoaji wa haki miongoni mwa jamii pana ya kitanzania sasa kama ina kabiliwa na tuhuma nzito kama hizo halafu wahusika wanakuja na majibu mepesi inatulazimisha kuamini kuwa tuhuma hizo ni za kweli.

Tatizo kubwa linalotukabili Watanzania sasa ni kwamba hata wataalamu wetu wa kutegemewa  wamegeuka kuwa wanasiasa na kusahau miiko ya taaluma zao huku wengi wao wakikubali kuwa wafuasi wa wanasiasa.

Wamekuwa ni watu wa kupokea maagizo  toka kwa wanasiasa wakielekezwa namna ya kujibu majibu ya kisiasa badala ya kutoa majibu ya kitaalamu kama taaluma zao zinavyo wataka wawe.

Imefikia wakati Watanzania wameanza kupoteza imani na mihimili hii ya mahakama na hii ni kutokana na kwamba  katika siku za hivi karibuni muhimili huu umekuwa ukilalamikiwa kwa mambo mengi kama vile rushwa na mambo mengine mengi.

Na hii ndiyo  maana katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia idara hii nyeti ya mahakama ikikubali kutumiwa na wanasiasa ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao kuwa kimbilio lao la kuzuia watu kudai haki zao.

Ifike wakati kila idara ijitambue kwa umuhimu wake na wahusika waheshimu taaluma zao na kamwe wasiruhusu kuingiliwa kiurahisi na wanasiasa wanaotumia nafasi zao kuendeleza kudumisha undugu na urafiki.

Wataalamu wetu hawa wasiwe waoga kukemea maovu kwa lengo la kulinda nafasi zao kwani kwa kufanya hivyo wanachangia kwa kiwango kikubwa kwao kuonekana miongoni mwa jamii kuwa hawafai.

Inawezekana tuhuma hizo zilizotolewa na msemaji huyo wa Idara ya Sheria na Katiba bungeni zikawa za kweli au uongo, lakini Watanzania wangetarajia kupata majibu ya kuridhisha toka kwa wahusika kulingana na umuhimu wa idara husika.

Wataalamu wetu hawa ni bora wakajua kuwa Taifa la Tanzania lipo mikononi mwao na inawezekana kutokana na udhaifu wao ndio maana leo tumefika hapa tulipo.

Hebu angalia mikataba mibovu iliyoingiwa na wanasheria wetu hawa huu ni ishara nyingine tosha ya madai ya Bw. Lissu kuwa idara hii imejaa watu ambao hawana sifa ila na waliopatikana bila ya kufuata taratibu za mamlaka husika.

Idara hii kwa kuzidi kukumbatia madhaifu yake ni kuwa inaidhalilisha jamii nzima ya watanzania inayo wahudumia kwa kuwalipa mishahara na marupurupu wanayo stahili kupewa.

Wamebaki kuwa wafanyabiashara wenye kampuni ya uwakili wanao watoza Watanzania gharama kubwa za kesi ilihali kumbe hawana hata sifa za kuitwa wanasheria hakika huu ni usaliti kwa Watanzania.

Na mwisho naomba kuiasa idara husika ikae ikijua kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote si yao peke yao kwa hiyo wanapo shindwa kuitetea taaluma yao ni sawa na kujidhalilisha wao wenyewe.

Kwani tabia hii ya kinafiki inatufanya tuwe nchi kubwa lakini sawa na taifa dogo, hatuna budi kubadilika na kujenga moyo wa kizalendo na tuisikie sauti ya watanzania ikikemea maovu duniani bila ya kumuogopa mtu yeyote kwa kuangalia wadhifa alionao kwa wakati huo, tafakari
0753-608480.

No comments:

Post a Comment