19 November 2012

Huu ni wakati wa Waafrika kuamka



Na Michael Sarungi

NIWAZI kuwa Bara la Afrika tangu karne ya 15 limepoteza mwelekeo na hivyo kuruhusu kuburuzwa katika kila mfumo unaoasisiwa na mataifa toka Ulaya na Marekani.


Kwa kiwango kikubwa hali hii imechangiwa na viongozi wetu kushindwa kabisa kuandaa mazingira ya utayari, ushirikishwaji na zaidi msimamo wa pamoja wa bara hili kwenye masuala ya kimataifa.

Kwa mfano ukianza kuyaangalia mataifa yaliyo mengi katika bara hili la Afrika ni kuwa mpaka hii leo mengi hayafahamiki yapo katika mfumo gani wa uzalishaji.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukishuhudia mataifa ya Ulaya yakiendelea kustawi ndani ya ubepali unaobeba utandawazi  na kupiga hatua za dhati kiuchumi miongoni mwa watu wao.

Cha kushangaza ni kuwa mataifa yetu ya Kiafrika nayo bila ya kutafakari yamekuwa yakijinadi kuwa yamo ndani ya mfumo huo wa kiutandawazi na haieleweki ni kwa mfumo na misingi ipi.

Labda niwaulize swali rahisi hawa watawala wetu ni nchi gani ya Kiafrika ambayo imetandawazi huko kwa wenzetu wanaotulazimisha kuwa watandawizi huu uchwara wa wazungu?

Afrika inahitaji kubadilika kuanzia kwa viongozi wetu mpaka kwa wananchi wa kawaida tusiwe watu wa kupokea vitu pasipo kwanza kufikiria madhara yake ya siku zijazo.

Tumeipokea dhana hii ya 'utandawizi' wa wazungu bila hata ya kufanya tathmini ya kina kama kweli tulikuwa tayari kuupokea mfumo huu na je watu wetu tuliwapa elimu ya kutosha juu ya dhana hii ya 'utandawizi' jibu ni hapana na matokeo yake tunayaona leo.

Ni bora Waafrika wakaelewa kuwa kwenye dhana hii ya 'utandawizi' sisi ni waathirika wakubwa na ni dhahiri kuwa tumebanwa vya kutosha na hatuwezi kujiondoa kiurahisi.

Utazungumziaje dhana ya 'utandawizi' kwa wanavijiji wa kiafrika ambao mpaka hii leo wakimuona mzungu wanashangaa kana kwamba wamemuona Mungu hiki si ni kichekesho?.

Labda swali la kujiuliza hapa ni kuwa chini ya dhana hii ya 'utandawizi' au utandawazi babu yangu kule katika Kijiji cha Isadukilo Magu vijijini ana nufaika na nini?

Leo tumeingizwa kwenye huo utandawazi
na matokeo yake kwa mwananchi wa kawaida tumeyaona badala ya kupata faida matokeo yake ni wengine kuondolewa kwenye makazi yao kwa lengo la kupisha wawekezaji walioletwa na utandawazi.

Kama hiyo haitoshi utandawazi huu ni katika nchi za Kiafrika tu mbona nguvu za Waafrika kuwekeza huko Ulaya, Amerika na kwingineko hazionekani hakika huu ni wizi wa mchana kweupe.

Labda swali la kujiuliza hapa ni kuwa nini hatima ya bara hili la waafrika katika miaka 100 ijayo wakati raslimali zetu na vitegauchumi vyetu vyote vitakapo kuwa mikononi mwa wageni?

Kwani tunacho shuhudia sasa ni viongozi wetu kukimbia na muda na si wakati na ndiyo maana mpaka hivi sasa kila wanachokifanya wanachojali ni saa zao tu na ndugu, marafiki na familia zao.

Wanashindwa kutambua kuwa katika maisha kuna nyakati za leo na kesho na wala hawafikirii kuwa kuna waafrika wengi nyuma yao wanaoishi kwenye lindi la umasikini wa kutupwa.

Leo hii haya maswala ya uwekezaji na huu unaoitwa uwekezaji yaliyo chini ya dhana ya utandawazi yanachukuliwa kwa masihara lakini ni ukweli ulio wazi kuwa yanatekelezwa kwa shingo upande kwa ni kazi hii haikuwashirikisha wananchi wa nchi hizi.

Waafrika wanalazimishwa kuuza kila kitu walichonacho kwa wageni kwa kisingizio cha dhana hii ya utandawazi kibaya hata viongozi nao wamebaki kuwa ni makuhadi wakubwa wa dhana hii.

Wanashindwa kujionea hata kwa macho kuwa hakuna uwiano wowote kati ya kile kinachovunwa na kampuni hizi za  kibepari na kile kinachobaki kwenye nchi husika.

Suala hili linakuja kuwa chanzo cha machafuko kwenye nchi zetu hizi za Kiafrika kwani historia toka kwenye nchi nyingi zinaonesha kuwa wawekezaji hawa wamekuwa ni watu wa kuvuna raslimali bila ya kujali hali ya nguvu kazi wanazo zitumia kuzalisha mali.

Kwa sasa tumeshuhudia waafrika wakitumia njia kama migomo midogo midogo na maandamano kwa lengo la kufikisha ujumbe wao mahali husika lakini huko mbeleni inaweza kuwa njia nyingine itakayo kuja kuleta hali ya mtafaruku mkubwa duniani.

Hapa ndipo tunapo ona kwa kiwango gani busara za kweli bado zinahitajika ili kuweza kuliokoa jahazi hili linaloendelea kuzama kila kukicha bila hata ya juhudi za kuliokoa.

Kwa maana nyingine ni kuwa picha hiyo niliyojaribu kuielezea hapo juu ni tatizo kubwa katika bara hili la Afrika na inawezekana madhara yake yasionekane sasa lakini ni hatari huko mbele ya safari.

Afrika inatakiwa kuwa na sauti moja hususan kwenye masuala nyeti yanayo gusa mslahi ya waafrika vinginevyo hali itazidi kuwa ngumu kila kukicha.

Mfano mmoja wa udhaifu uliodhihirishwa na waafrika na umoja wao ni mahasibu yaliyoikuta nchi ya Zimbabwe na wote tumeshuhudia yaliyo tokea kwa wananchi wa nchi hiyo.

Hebu itazame Zimbabwe ya leo huwezi kuamini kama kweli ndiyo Zimbabwe tunayo ifahamu mfumuko wa bei ulipanda mpaka kufikia asilimia 500, uchumi ukazidi kuwa duni kiasi cha wananchi kuishi maisha magumu na ya kutisha, lakini hakuna sauti ya maana iliyosikika kuwalaumu wazungu walio iwekea nchi hiyo vikwazo.

Mabepari wameiwekea vikwazo nchi hiyo kila kona huku mataifa ya Afrika yakiwa yamelala usingizi wa pono huku wengi wakishirikiana na kampuni za wazungu kupora raslimali za nchi zao wenyewe.

Kukosekana huko kwa umoja wenye nguvu katika bara hili kumesababisha wazungu kutupangia kila kitu nasi kuwa ni watu wa kupokea kila kitu na kutekeleza bila hata ya kuwa na uwezo wa kuhoji.

Kwa kutambua pungufu wetu, wazungu wamebuni njia nyingine ya kuja kuitawala Afrika kwa kutumia dhana ya utandawazi na kwa kujitambua au kutojitambua viongozi wamekubali kuwa makuhadi na kuwasahau wafuasi wao.

Viongozi wetu wamelazimika kukumbatia sera na mipango kandamizi toka Ulaya na Marekani baadhi yao wamekata tamaa na hivyo kuwa wavunaji wa mali binafsi.

Wengi wao wanashindana kuwekeza mali walizoiba toka kwenye nchi zao huko Ulaya na kwingine duniani kwa lengo la kuwafaa ziku zijazo na familia zao, marafiki na wengine wanao wazunguka.


Na mwisho nimalizie makala hii kwa kuwaasa viongozi wetu hawa wa kiafrika kuwa hakuna njia nyingine binafsi zaidi ya kuangalia uhuru wa nchi hizi za kiafrika wanaodai kuwa nao.

Na zaidi ni bora kuuvaa Uafrika,uzalendo na kuweka kando roho za kibinafsi katika kuhakikisha kuwa bara hili lina kuwa na sera zake, mipango na misimamo ya pamoja kuliko kukubali kila kitu wanacholetewa toka Ulaya na Marekani, tafakari




No comments:

Post a Comment