19 November 2012

Tukio la kutoroka mfungwa gerezani tunahitaji majibu



JESHI la Polisi nchini linafanya jitihada kubwa za kupambana na uhalifu pamoja na wahalifu ambao ni kikwazo cha maendeleo ya wananchi kutokana na nguvu wanayotumia kutaka utajiri wa
haraka wasioutolea jasho hata kusababisha vifo.

Wakati jeshi hilo likifanya kazi ya kupambana na uhalifu usiku
na mchana katika mazingira yanayohatarisha maisha ya askari,
inasikitisha leo hii watuhumiwa wanaokamatwa na kufungwa gerezani, wanatoroka katika mazingira tata.

Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Salum Msangi, jana alitoa taarifa za kukamatwa mfungwa ambaye bado anatumikia kifungo cha miaka 15 gerezani, baada ya kuhukumiwa mwaka 2010.

Mfungwa huyo Bw. Masanja Maguzu (42), mkazi wa Kijiji cha Ng’wang’wali, alikutwa nyumbani kwake akiwa na silaha za kivita ikiwemo bunduki aina ya SMG, yenye risasi 31 pamoja na magazini tatu, moja kati ya hizo ni ya bunduki aina ya Uzi Gun.

Inaelezwa kuwa, Bw. Maguzu alihukumiwa kifungo hicho mwaka 2010, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Shinyanga baada ya kukutwa na bunduki aina ya SMG, iliyokuwa na risasi 622.

Mbali ya kukamatwa mfungwa huyo, Kamanda Msangi alidai jeshi hilo linafanya uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira ambayo yamesababisha awe nje ya gereza wakati muda wa kutumikia kifungo hicho bado mchanga.

Tukio la kukamatwa mfungwa huyo akiwa uraiani wakati muda wa kutumikia kifungo chake haujaishi ni aibu kwa Jeshi la Magereza ambalo linapaswa kutoa maelezo ya kina kwa jamii.

Hii inaonesha ni jinsi gani magereza yetu yasivyo na ulinzi makini wa kuwalinda watuhumiwa waliohukumiwa vifungo badala yake wanatoroka mikononi mwao na kwenda kuendeleza uhalifu katika maeneo mbalimbali hata kusababisha vifo.

Mara nyingi taarifa za wafungwa au mahabusu wanapotoroka magerezani huwa zinatolewa kwenye jamii ambayo hushirikiana
na jeshi la Polisi kuwasaka ili wasiendelee kuleta madhara.

Katika hili hakuna taarifa iliyotolewa na Jeshi la Magereza hivyo kuifanya jamii iamini kuwa, yapo mambo mengi yanayofanyika magerezani lakini taarifa zake zipo nyuma ya pazia.

Sisi tunasema kuwa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wafanye uchunguzi wa kina ili wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kumtorosha mfungwa huyo, wabainike
na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Yawezekana wahalifu wengi wanaosumbua katika maendeleo mbalimbali nchini wametoroka katika magereza waliyofungwa
bila taarifa zao kuwekwa hadharani hivyo kuhatarisha usalama
wa wananchi na mali zao.

No comments:

Post a Comment