29 November 2012

TBS, wadau wajadili viwango lisha ya watoto


Na Rachel Balama

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS)na wadau mbalimbali wanaojishughulisha na lishe nchini wamekutana kujadili viwango saba katika lishe na chakula kwa ajili ya matumizi maalum ya watoto vitakavyotumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara cha  Chakula, Sayansi na Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa Joyce Kinabo, alisema mkutano huo wa siku mbili utajadili viwango vya vyakula kwa watoto walio chini ya mwaka mmoja na zaidi.

"Tunaingia kwenye soko la pamoja hivyo tunaandaa msimamo wa Tanzania katika viwango ambavyo vitashirikisha kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki," alisema Prof. Kinabo.

Alisema hatua hiyo itawasaidia watumiaji pamoja na wafanyabiashara kuwa na uhakika wa chakula ambapo wanajadili viwango saba.

Akifungua mkutano huo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS) Leandri Kinabo,alisema mkutano huo ni maandalizi ya mkutano utakaofanyika nchini Rwanda utakaoangalia viwango vya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Lengo la mkutano huu ni kujadili viwango vya lishe na chakula ikiwa pia ni maandalizi ya mkutano kama huu utakazikutanisha nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki," alisema.

Alisema kuwa kabla hawajakutana na wataalumu wa viwango kutoka nchi za Afrika Mashariki wameamua kuangalia viwango vya Tanzania kama vinaweza kukithi soko la pamoja.

Kwa upande wake Meneja wa Viwango, Tumaini Mtitu,aliwataka wadau hao kuangalia kwa makini viwango hivyo kwa manufaa ya Watanzania wote.

No comments:

Post a Comment