29 November 2012

SUMATRA yapokea maoni ongezeko la nauli



Na Leah Daudi

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini(SUMATRA),imepokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu mapendekezo ya ongezeko la nauli kwa mabasi yaendayo mikoani.


Akizungumza katika mkutano huo Kaimu Mkurungenzi Mkuu wa SUMATRA Dar es Salaam jana, Bi.Tumaini Silaa alisema madhumuni ya kuwakutanisha wadau wa sekta ya usafiri wa barabarani kupata maoni kutoka kwa wadau kuhusu maombi ya nyongeza katika nauli ya mabasi yaendayo mikoani kama zilivyowasilishwa na Wamiliki wa Makampuni ya Mabasi ya ABC Trans na Happy Nation.

Bi.Silaa alisema kuwa Sumatra ipo kwa ajili ya kusimamia suala la mtoa huduma na mtumiaji wa ili kutimiza mahitaji ya pande zote mbili na kutafuta uwiano.

"Hatuna budi kuwasikiliza wadau ili tuweze kutoa maamuzi ambayo yana manufaa kwa pande zote mbili na kuboresha huduma," alisema.

Alisema kuwa katika mkutano huo hawatatoa jibu kuhusiana kiwango cha juu cha nauli kinachoruhusiwa kutozwa na wasafirishaji wa mabasi ya kwenda mikoa lakini kupitia michango ya wadau itakuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza maoni yao kisheria.

"Itakaposikika kuwa mwenye kampuni anatoza nauli iliyo juu ya ile itakayopitishwa au ile ilyopo ataadhibiwa bila huruma ikiwa ni pamoja na kumfungia leseni," alisema.

Alisema kuwa wataimarisha ushirikiano wa karibu zaidi na wananchi na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha wale wote wanaokiuka sheria na kusababisha ajali watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment