29 November 2012

Serikali yaombwa kusimamia mfumuko wa bei za vyakula


Na Rose Itono

WANANCHI wameiomba serikali kusimamia bei za bidhaa ili kuwapunguzia mzigo mkubwa wananchi kutokana na kupanda kwa bei kiholela.


Wakizungumza na Majira Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi walisema kuwa, bidhaa za chakula katika kipindi hiki zimepanda kwa kasi na kusababisha mzigo mkubwa kwa wananchi.

Bw.Juma Dikwe mfanyabiashara wa nafaka katika soko la Tandale alisema kuwa kupanda kwa bidhaa hizo kunatokana na uhaba wa mvua.

Alisema awali walikuwa wakiuza mchele kwa bei ya rejareja kwa sh.1000 hadi 2000 lakini kutokana upungufu wa bidhaa hiyo kutoka kwa wakulima wamelazimika kupandisha bei na kuuza kilo moja kwa sh.1800 hadi 2500.

Alisema kwa upande wa unga bei ya awali ilikuwa ni sh. 800 hadi 1000 kwa kilo lakini sasa hivi bei imepanda na kufikia Sh.1200 hadi 1500 ambapo maharage ya Mbeya yaliyokuwa yakiuzwa kwa Sh.1600 kwa kilo sasa hivi huuzwa kwa sh.2500 hadi 3000.

Mkazi wa Kiwalani Bi.Joan Mathew alisema kuwa kupanda kwa gharama za chakula kumefanya baadhi ya wananchi hasa wa kipato cha chini kula milo miwili kwa siku.

Aliishauri Serikali kupitia wizara husika kusimamia kikamilifu suala hilo ili kuweza kunusuru maisha ya watu hasa wa kipato cha chini.

Hata hivyo hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imewaatharisha wananchi kutumia maji kwa uangalifu na kuhifadhi malisho kwa ajili ya mifugo kutokana na mvua ndogondogo zilizonyesha chini ya wastani hadi sasa.

Kwa mujibu wa Ofisa habari wa TMA Bi.Monica Mutoni alisema kuwa,upo uwezekano wa kuwepo vipindi vifupi vya mvua kubwa hivyo wananchi wanashauriwa kuendelea kuchukua tahadhari.

Taarifa ilisema kipindi cha Julai hadi Septemba hali ya joto la bahari katika ukanda wa Tropikali wa bahari ya Pasifiki iliongezeka na kuwa juu ya wastani,hivyo kuashiria uwepo wa mvua hafifu za El Nino ambapo hali ya mifumo ya upepo mgandamizo wa hewa katika usawa wa bahari na mawingu.

No comments:

Post a Comment