19 November 2012

RC aagiza mazao ya wananchi kufyekwa Veronica Modest na Timothy Itembe, TarimeMKUU wa Mkoa wa Mara, Bw. John Tuppa, ameuagiza uongozi
wa Wilaya ya Tarime, kufyeka mazao yote yaliyomo na wananchi katika eneo ambalo linamilikiwa na Serikali ili kuondo migogoro
ya ardhi ya wakazi wa Kijiji cha Ng’ereng’ere na Kurutamba.


Bw. Tupa alitoa agizo hilo juzi baada ya kufanya ziara ya kukagua eneo hilo ambalo linasababisha machafuko ya mara kwa mara kati ya wakazi wa vijiji hivyo.

Alisema awali eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na wananchi lakini kutokana na migogoro kugombania mipaka iliyokuwa ikijitokeza kwa wakazi wa vijiji hivyo, waliamua kulikabidhi kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mwaka 2004.

“Eneo hili lilikabidhiwa kwa JKT ili kuepusha migogoro ambayo iliyokuwa ikijitokeza, wakazi wa vijiji hivi walikuwa wakifanya shughuli za kilimo katika eneo hili kinyume cha sheria,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuuagiza uongozi wa Wilaya hiyo, kuhakikisha wote wanaochochea mapigano kuanzia madiwani, wazee wa kimila  na waliohusika katika mauaji ya mwananchi mmoja hivi karibuni, wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.

“Viongozi wa kitongoji na kata zote, tunaomba mfuate taratibu, kama mngezifuata tangu awali tusingekuja hapa, matatizo haya yangekuwa yameisha kwani tumechoshwa na migogoro hii.

Kwa upande wao, wahanga wa mgogoro huo katika Kijiji cha Nyamaraga, waliiomba Serikali kuingilia kati ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo lililopo kwani hata wao wamechoshwa na mapigano ya mara kwa mara na wanachokitaka sasa ni maendeleo.

Waliiomba Serikali iwekeze mradi wowote katika eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 193.3 ambalo ndio chanzo cha migogoro ya mara kwa mara kwani lina rutuba nzuri hivyo kuwavutia wananchi na kulitumia kwa kilimo cha mazao ya chakula.

“Tangu mwaka 1992, eneo hili limekuwa chachu ya mapigano kati ya koo mbalimbali hivyo umefika wakati wa Serikali kuchukua hatua za haraka ili kunusuru vifo vinavyoweza kutokea,” walisema.

Diwani mstaafu wa kata hiyo, Bi. Magreti Mwikwabe, alisema chanzo cha migogoro hiyo ni baada ya ramani ya eneo hilo kuandaliwa upya na kuacha mipaka ya zamani ya Ingirimi.

Wakazi wa vijiji hivyo walipokea tamko la Mkuu wa Mkoa kwa hisia tofauti na kudai walipaswa kupewa muda ili waweze kuvuna mazao yao ndipo utekelezaji huo uanze mara moja.

No comments:

Post a Comment