19 November 2012

Lowassa: Elimu ya sekondari iwe bureNa Mwandishi Wetu, Babati

WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Edward Lowassa, amesema wakati umefika wakati wa Serikali ya Tanzania kutoa elimu ya sekondari bure ili wazazi waondokane na mzigo walionao.

Bw. Lowassa aliyasema hayo mjini Babati, mkoani Manyara kabla ya kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Usharika wa Babati.

Katika harambee hiyo, zilihitajika sh. milioni 120 ili kufanikisha ujenzi huo ambapo zaidi ya sh. milioni 186, tayari zimetumika ambapo gharama halisi za ujenzi huo ni sh. milioni 600.

Alisema khivi sasa kila kata nchini ina shule ya sekondari ambapo huo ulikuwa mpango akiwa Waziri Mkuu na alisimamia kikamilifu suala hilo na kufanikiwa kwa asilimia 100.

Bw. Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Monduli, mkoani Arusha, alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kulizungumzia suala hilo bila woga hasa wadau wa elimu.

“Lazima tukubali na tujadili suala hili kwa manufaa ya nchi, kila Mtanzania akubali ushauri wa elimu ya sekondari kutolewa bure,
Serikali inapaswa kugharamia elimu ya sekondari bila woga na mwananchi anapaswa kuchangia mahitaji mengine kama kupata elimu ya Kilimo Kwanza kwani sekta hiyo ndio uti wa mgongo
wa nchi yetu,” alisema Bw. Lowassa.

Alisema hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete alitoa wito kwa shule za sekondari kujenga maabara kwa wingi ambapo suala hilo linapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote pamoja na lile la elimu ya sekondari kutolewa bure.

“Elimu ya sekondari itolewe bure kama tunavyofanya katika elimu ya msingi, watoto wasome bure kuanzia kidatu cha kwanza hadi cha nne, wadau mbalimbali nchini wawe mstari wa mbele kuchangia elimu ili siku za baadae, nchi iwe na vijana wenye elimu nzuri,” alisema.

Akizungumzia tuhuma zinazoandikwa katika mitandao na magazeti kuwa yeye ana utajili wa kutisha, Bw. Lowassa alisema madai hayo hayana ukweli wowote kwani kuchangia shughuli za maendeleo sio kosa kwani anapofanya hivyo kushirikisha marafiki zake.

Alisema anachokifanya katika shughuli anayoalikwa, huwajulisha rafiki zake kote nchini ili watoe michango yao hivyo hana utajiri wowote kama inavyodaiwa katika mitandao bali ataendelea kutoa michango na marafiki zake ambapo tuhuma hizo hazimtishi.

Naye Askofu Mkuu wa KKKT, Kanda ya Kaskazini na Kati, Dkt. Thomas Laizer, aliwataka waumini wa kanisa hilo kote nchini na wale wa makanisa mengine, kuwapuuza baadhi ya watu ambao wanataka kuleta furugu nchini.

Alisema vurugu za kuchoma makanisa kama ilivyotokea Mbagala na maenmeo mengine zinapaswa kupuuzwa na kuwataka waumini wa kamanisa hayo kutolipiza kisasi kwani huo si utamaduni wa dini ya Kikristo.

Aliongeza kuwa, wapo Waislamu wasiopenda vurugu na kuwaomba Watanzania wote kuombea amani iliyopo isipotee pamoja na kuendeleza mshikamano uliopo.

“Kila mtu mwenye dini afanye maombi kuiombea nchi yetu amani, yapo makanisa mengi yamechomwa moto si kwamba waumini wa dini ya Kikristo ni waoga, la hasha, utamaduni wa dini yao unakataza kulipiza kisasi,” alisema.

No comments:

Post a Comment