26 November 2012
Polisi Dar wakamata majambazi sugu watano
Zubeda Mazunde na Angelina Faustine
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata majambazi sugu watano wakiwa na silaha mbalimbali za moto walizokuwa wakizitumia kufanya matukio ya uhalifu na mauaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema majambazi hao wote ni wakazi wa jiji hilo.
Alisema kukamatwa kwa majambazi hao kumetokana na msako mkali uliofanywa na jeshi hilo ambapo mbali ya kukutwa na silaha hizo pia walikutwa na magari matano ya wizi kati ya hayo mengine yalikuwa na namba batili.
“Magari haya walikuwa wakiyatumia kufanya uhalihu katika maeneo mbalimbali na majina yao ni Peter Godfred (30), mkazi
wa Mbagala, Majid Ungaunga (25) Hamis Hassan (32), wote
wakati wa Vingunguti, Amini Salehe (30) na Niclous Dismas
(30), wakazi wa Tegeta,” alisema Kamanda Kova.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kova aliwahadharisha wananchi kutofanya vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuwaweka katika mazingira magumu hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Alisema Jeshi la Polisi limeandaa mpango kabambe wa kupambana na uhalifu pamoja na wahalifu wanaotumia silaha, kuvunja maduka na kubadilisha fedha bandia katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Aliwataka waendesha pikipiki kuhakikisha wanavaa kofia ngumu, wanapoendesha vyombo vya moto ili waepukane na madhara makubwa yanayoweza kuwapata kichwani kama itatokea
watapata ajali za barbarani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment