26 November 2012

CCM wataka M/kiti Chadema aburutwe kortini



Na Mwandishi Wetu, Geita

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Katoro Mazemule, mkoani Geita na wenzake wanaodaiwa kuhusika na wizi wa sh. milioni 16.5 za halmashauri
ya kijiji hicho, wafikishwe mahakamani haraka.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara jana, uliofanyika katika Mji Mdogo wa Katoro, mkoani humo, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye, alisema fedha hizo zimetokana na jasho la wananchi hivyo lazima wahusika wafikishwe mahakamani.

Fedha hizo zinadaiwa kuliwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),  kipindi cha mwaka 2010/11, hivyo kuzusha tafrani miongoni mwa wananchi na uongozi wa halmashauri ya kijiji hicho hadi sasa.

Bw. Nnauye alisema kamati iliyoundwa kuchunguza upotevu wa fedha hizo tayari ilimaliza kazi yake na ripoti ya uchunguzi wao kukabidhiwa kwa mamlaka zinazohusika.

“Kamati ya kuchunguza wizi wa fedha hizi ambazo ni mali ya wananchi ilishafanya kazi yake na kukabidhi ripoti kwa mamlaka zinazohusika, nini kinachokwamisha wahusika hawa wasipelekwe mahakamani hasi sasa.

“Kwa kuwa CCM ndio chama tawala, tunaagiza hatua za wahusika wote kupelekwa mahakamani zichukuliwe haraka ili haki iweze kutendeka,” alisema Bw. Nnauye.

Alisema kitendo cha wizi huo kufanyika chini ya watendaji wa chama hicho ni dalili tosha kuwa majigambo yao ya kuwa wasafi
na wapigania haki za wanyonge ni sawa na kilio cha mamba.

“Kila mara tumekuwa tukiwaambia msidanganywe na CHADEMA, kwani si chama cha siasa bali ni kundi la wajanja, sasa wana Katoro mmejionea wenyewe, mmewajaribu mkawapa halmashauri yenu, fedha wamezitafuna sasa mnahangaika.

“Kwa kuwa mmepata funzo, bila shaka hamtaruidia tena kwani mtakuwa na picha kamili kuwa mkiwapa uongozi CHADEMA
ni sawa na kumkabidhi fisi bucha,” alisema Bw. Nnauye.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Geita, Bw. Joseph Msukuma, alisema kama hatua za kuwafikisha mahakamani wahusika hazitachukuliwa haraka, atawaongoza wananchi hao kuandamana ili kuhakikisha hatua hizo zinachukuliwa.

Kabla ya mkutano huo, Bw. Nnauye alifungua shina la wajasiriamali la CCM, Bugayambele lenye wanachama  53 ambao linajihusisha na kazi ya kutengeza fenicha mbalimbali.

Bw. Nnauye aliahidi kuwapa sh. milioni moja ili waendeleze shughuli zao pamoja na kununua vitendea kazi kama randa za
mbao na ujenzi wa banda la kisasa.

No comments:

Post a Comment