21 November 2012

Mradi wa LVEMP 11 mkombozi wa mazingira Ziwa Victoria


Na David Mihambi

WAZIRI wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, hivi karibuni alikuwa jijini Mwanza kwa ajili ya kukabidhi magari ya mradi wa Hifadhi Mazingira ya Ziwa Victoria (LVEMP 11)ambayo yatatumika katika kuongezea utendaji wa watumishi wa mradi huo.

Mwandishi Jovin Mihambi alipata fursa ya kuongea naye kuhusiana na maendeleo ya mradi huo.

Swali:Mheshimiwa waziri, hebu niambie madhumuni ya mradi wa Hifadhi Mazingira ya Ziwa Victoria (LVEMP 11)

Jibu:Mradi wa Hifadhi Mazingira ya Ziwa Victoria awamu ya pili ni mradi ambao unasimamiwa na Wizara yangu  na ulianza rasmi Agost 20, 2009 na unatekelezwa kwa kushirikiana na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Nchi hizo ni Burundi, Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda na lengo lake  kubwa ni kuimarisha usimamizi shirikishi wa rasilimali za Bonde la Ziwa Victoria na kupunguza athari za uharibifu wa mazingira katika ziwa letu.

Swali:Nini madhumuni ya kuanzishwa kwa mradi wa LVEMP 11.

Jibu: Mradi wa LVEMP 11 ulianza kutekelezwa mnano Septemba, 2009 na ulipangwa kutekelezwa katika awamu mbili za miaka minne kila mmoja,yaani sehemu ya kwanza kuanzia mwaka 2009 hadi 2013 na sehemu ya pili kuanzia 2013 hadi 2017.

Swali:Fedha za kuendesha mradi zinatoka wapi?

Jibu: Fedha za kuendesha mradi zinachangiwa na serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia (WB) na jamii husika.

Aidha shughuli za kikanda chini ya Jumuia ya Afrika Mashariki zinafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Mazingira (GEF) na Shirika la Maendeleo la Swenden (SIDA) na bajeti ya Mradi kwa sehemu ya kwanza ni dola za Marekani takribani milioni 32.5.

Swali:Malengo mahususi ya mradi wa LVEMP 11 ni yapi

Jibu: Ni kuimarisha uwezo wa usimamizi shirikishi wa rasilimali za Bonde la Ziwa Victoria hususani maji na samaki, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mbali na hilo pia lengo jingine ni kupunguza matatizo ya uchafuzi wa mazingira yanayotoka katika maeneo ambayo ni vyanzo vikuu vya uchafuzi
na pia katika maeneo ya vyanzo vya maji vilivyoharibiwa.

Swali:Ni sababu zipi ambazo zimesababisha mradi huu uingie katika awamu ya pili baada ya awamu ile ya kwanza muda wake kumalizika.

Jibu: Wakati wa awamu ya kwanza ya mradi huo unaanza,wizara yangu awali ilikuwa inakabiriwa na changamoto nyingi za uhifadhi wa mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria ambazo kabla ya mradi tulikuwa tunakabiliana nazo na baada ya mradi huo kwa awamu ya kwanza kumalizika.

Pamoja na kuwa changamoto hizo zilipungua kwa kiasi asilimia 90, nimeona kuwa mradi huo lazima uwe endelevu kutokana kwamba baadhi ya matatizo juu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira katika ziwa Victoria mengine yamekuwa yakijirudiarudia.

Swali:Ni matatizo gani ambayo baada ya awamu ya kwanza ya mradi wa LVEMP 1 kumalizika ambayo yamekuwa yakijirudiarudia na kusababisha kuendelea kuwepo uchafuzi wa mazingira.

Jibu: Kumekuwepo na tatizo kubwa la uvuvi usio endelevu na unaotumia zana hatari na zisizoruhusiwa kisheria.

Pia tatizo jingine ni upungufu wa taarifa sahihi kuhusiana na njia salama za kupitia meli na vyombo vingine vya majini pamoja na vifaa vya kuonesha njia hizo.

Pia kutokuwepo na mfumo wa pamoja wa kudhibiti utiririshaji wa maji kutoka kwenye Ziwa Victoria kwa mahitaji mbali mbali kwa nchi zote husika na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha kushuka.

Swali:Mbali na changamoto hizo, kwa upande wa kilimo na ufugaji, ukataji miti hovyo usiozingatia hifadhi mazingira kwenye vyanzo vya mito hilo unalielezeaje.

Jibu: Changamoto za uharibifu wa mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo ni pamoja na uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, usafirishaji, uzalishaji.

Changamoto nyingine ni viwandani, uchimbaji madini na utiririshaji wa maji kutoka viwandani hadi katika ziwa ambayo hayachujwi kwa ajili ya kuondoa taka na kemikali nyingine.

Pia mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha kushuka kwa kina cha maji na athari nyinginezo nyingi.

Swali:Kwa upande wa Tanzania ni maeneo gani ambayo yamelengwa katika kufanikisha mradi huu wa LVEMP 11

Jibu: Kwa upande wa Tanzania, maeneo yatakayofanyiwa kazi na mradi huo ni pamoja na kuimarisha taasisi zinazohusika na hifadhi ya maji na samaki kujenga au kukarabati mifumo ya kusafisha majitaka katika miji mikubwa ambayo iko kando kando ya Ziwa Victoria.

Miji hiyo ni Mwanza, Musoma na Bukoba na pia kuhifadhi mkondo wa  Mto Simiyu kwa kuanzisha miradi midogo ya jamii ya kuboresha mazingira na kuinua kipato kwa wananchi wa eneo hlo.

Swali:Mpaka sasa na jumla ya miradi mingapi inatekelezwa na Mradi wa LVEMP 11

Jibu: Kwa kuzingatia utaratibu wa hifadhi mazingira ya Ziwa Victoria, jumla ya miradi midogo 89 ya jamii yenye thamani ya Sh. bilioni 2.5 za kitanzania inatekelezwa katika maeneo ya mradi yenye lengo la kuhifadhi mazingira na kuongeza kipato cha wananchi wa Tanzania.

Na hii ni hatua kubwa sana na serikali itahakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kukidhi matarajio ya walengwa.

Swali:Katika mwaka huu wa fedha 2012/2013 serikali imetenga kiasi gani cha fedha katika kuibua miradi mingine mipya katika mpango wa LVEMP 11

Jibu: Katika mwaka huu wa fedha wa 2012/2013, mradi umepanga kuibua na kutekeleza miradi mingine midogo midogo ipatayo 100 yenye thamani ya Sh.bilioni 3 katika halmashauri zote zinazopakana na Ziwa Victoria.

Aidha, mradi utatekeleza kazi ya ujenzi na ukarabati wa miondombinu ya kusafisha majitaka katika miji ya Mwanza na Bukoba.

Pia miradi hii ambayo imesambaa katika wilaya tano za mkondo la mto Simiyu na nyingine sita za wilaya zinazopakana na ziwa zinahitaji nyenzo za kutosha ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wake unakamilika kwa ufanisi zaidi.

Swali:Je, ni vitendea  kazi vipi  ambavyo tayari mradi wa LVEMP 11 umekwishapokea kutoka kwa wahisani ili kurahisisha watendaji katika mradi huu kufanya kazi bila ya matatizo.

Jibu: Kwa kuzingatia umuhimu wa kuwepo na vitendea kazi, mradi huu tayari umekwishakabidhi pikipiki 21 kwa halmashauri za wilaya na taasisi mbali mbali ambazo zinatekeleza mradi huu.

Naupongeza sana uongozi wa mradi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia  ambao ni wafadhilii wetu wakuu kwa kazi hiyo kubwa ya kuhakikisha kuwa watendaji kazi wanapata nyenzo za kufanyia kazi.

Vile vile mradi umenunua magari mapya 22 yenye thamani ya Sh. bilioni1.9 ambayo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa kwa ufanisi na unafikia malengo yaliyosubiliwa kwa hamu kubwa na wananchi wa eneo la mradi.

Magari hayo tayari yamekabidhiwa kwenye idara za serkali, taasisi za umma pamoja na Halmashauri za Wilaya za Maswa, Bariadi, Kwimba, Magu na Meatu.

Swali:Vifaa hivyo yakiwemo magari na nyenzo nyingine utahakikishaje kwamba zitatumika kufuatana na malengo ya mradi kama ilivyokusudiwa.

Jibu: Ndugu Mwandishi, napenda kukuhakikishia kwamba wizara yangu kama msimamizi mkuu wa mradi huu, itafuatilia kwa makini matumizi ya magari na nyenzo nyingine.

Na pale itakapobainika kuna matumizi yasiyoridhisha ya vitendea kazi hivyo, serikali haitasita kuchukua hatua zinazostahili ikiwa ni pamoja na kurejesha magari husika wizarani ili yapangiwe shughuli nyingine na wahusika kuchukuliwa hatua za kinidhamu.


No comments:

Post a Comment