21 November 2012

Mfanyabiashara aungua moto, afariki dunia Dar


Leah Daudi na Angelina Faustine

MKAZI wa Ukonga, Mazizini kwa Mkoremba, Wilaya ya Ilala,
Dar es Salaaam Denis Martini (42), ambaye ni mfanyabiashara, amefariki dunia baada ya kuungua na moto.


Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Komba, alisema tukio hilo limetokea juzi kwa Mkoremba ambapo marehemu aliwasha kibatari ambacho kililipuka na kushika godoro.

“Marehemu alikuwa usingizini, kibatari alichowasha kililipuka, kushika godoro na kuteketeza mali zote ambazo zilikuwa ndani
ya duka pamoja na yeye mwenyewe kuungua moto,” alisema.

Alisema baada ya tukio hilo marehemu alikimbizwa hospitali ya Amana Ilala lakini alifariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Kamanda Komba alisema, moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zima Moto kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo ambapo thamani ya mali iliyoungua bado haijafahamika.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Amana  ambapo upelelezi juu ya tukio hilo bado unaendelea.

Wakati huo huo, moto umezuka ghafla katika eneo la Stakishari Ilala, kwenye duka linalomilikiwa na Bw. Pascal Colnery (28),
na kuteketeza mali yote iliyokuwemo dukani.

Kwa mujibu wa Kamanda Komba, alisema thamani ya mali ambayo imeteketea bado hazijafahamika na chanzo cha moto huo inadaiwa ni hitilafu ya umeme na hakuna madhara yaliyotokea kwa binadamu.

No comments:

Post a Comment