21 November 2012

Mwenyekiti CCM Geita adaiwa kuwatisha wakaguzi MaliasiliNa Daud Magesa, Mwanza

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Geita, Bw. Joseph Kasheku, anadaiwa kuwatisha watumishi wa Kikosi Maalumu cha Maliasili na Misitu cha Kukusanya Maduhuli ya Serikali na kudai atawafukuzisha kazi baada ya kukamatwa na
mbao pamoja na vipande vya magogo zaidi ya tani tatu.


Mbao na magogo hayo yalikuwa yakisafirishwa na basi ambalo linamilikiwa na Mwenyekiti huyo kutoka Kata ya Runzewe, Wilaya ya Bukombe, mkoani humo kwenda jijini Mwanza, bila kuwa na nyaraka zozote ambapo baadhi ya mbao zilichukuliwa na Maofisa
hao kama kielelezo na kuzipeleka katika ofisi zao.

Akithibitisha kukamatwa kwa mbao na magogo hayo, kiongozi wa
Kikosi cha Ukusanyaji Maduhuli mikoa ya Mwanza na Mara, Bw. Ngatara Kimaro, alisema walipata taarifa kutoka kwa wenzao kuwa kuna shehena ya mbao na magogo ambayo ilikuwa ndani ya gari
la abiria ambalo lilikuwa likitokea Runzewe.

“Baada ya kupata taarifa hizi, tulilifuatilia basi husika lenye namba za usajili T 517 BBJ na kulisimamisha wakati likitoka kwenye kivuko cha Kamanga lakini dereva wake aligoma kusimama.

“Huyu dereva aliwasiliana na Bw. Kasheku ambaye alitupigia
simu na kudai atatufukuzisha kazi, gari lilikwenda kuegeshwa
nje ya karakana yao, tulipokwenda ili kutaka kulikagua
walikataa na kudai mwenye funguo hayupo,” alisema.

Bw. Kimaro alisema walilazimika kuwasiliana na Jeshi la Polisi
na wakati wakisubiri askari, ghafla mlango la kuingia ndani ya karakana ulifunguliwa na gari hilo kuingizwa ndani ambapo
polisi walifika eneo hilo jioni kusimamia ukaguzi huo.

“Baada ya polisi kuwasiri eneo la karakana, wafanyakazi wa basi hili walikubali tufanye ukagusi na kukuta mbao na vipande vya magogo vilivyopangwa kwa ustadi mkubwa, mbao nyingine zilikuwa chini ya uvungu wa viti vya abiria na kwenye keria,” alisema.

Aliongeza kuwa, mbao hizo hazikuwa na nyaraka zozote za uhalali wa kusafirishwa na walipozikagua zilionekana kuvunwa kinyume cha sheria kwa sababu hazikuwa na alama ya msitu.

Inadaiwa kuwa, Bw. Kasheku alizungumza kwa simu na Maofisa hao akiwazuia wasifanye kazi hiyo hadi alipwe nauli ya ubebaji
wa mbao hizo bila kumtaja mmiliki wake.

Alisema kwa mujibu wa sheria za usafirishaji, gari yake inaruhusiwa kusafirisha mizigo na abiria ambapo ile inayoshindikana kupakiwa kwenye buti inapakiwa kwenye lori.

Akizungumza na gazeti hili, Bw. Kasheku alisema suala la kutokuwa na nyaraka linahusu kitengo kingine na kupakia mbao ni jambo jingine kwani yeye ni mfanyabiashara anayesafirisha abiria na mizigo inayoweza kuingia kwenye basi,” alisema.

Aliongeza kuwa, basi hilo lilikaguliwa na Maoafisa misitu waliopo barabarani katika vituo tisa kutoka Runzewe Bukombe hadi Kamanga Sengerema.

No comments:

Post a Comment