30 November 2012

Mapigano Tegeta mmoja ajeruhiwa shavu la kushoto


Na Angelina Faustine

MKAZI wa Tabata, Bw. John Paulo (20), jana alipata majeraha katika shavu la kushoto wakati polisi walipopiga mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi katika eneo la Tegeta.

Wananchi hao wanadaiwa kukaidi agizo la kuondoa magari yaliyoegeshwa katika eneo la hifadhi ya barabara ambayo
hivi sasa ipo katika ujenzi unaofanywa na Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS).

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema mbali ya watu hao kukaidi agizo hilo pia waliwarushia mawe polisi waliokuwa eneo hilo
ambao walilazimika kupiga mabomu ya machozi ili kujihami.

“Katika vurugu hizo, huyo kijana aliumia katika shavu la kushoto na kukimbizwa Hospitali ya Mwananyamala, ila nasikitika kusema kuwa, baadhi ya vyombo vya habari vinaripoti matukio ambayo yanatokea katika jamii bila kuthibitisha,” alisema.

Alisema baada ya vurugu hizo, kituo kimoja cha televisheni nchini kiriripoti kuwa, kijana huyo amefariki dunia baada ya kupigwa na askari katika eneo la tukio jambo ambalo si kweli.

“Ni vizuri kuripoti habari zenye uhakika kutoka kwa wahusika wanaopaswa kutoa taarifa sio kuripoti, nawaomba wannchi muwe
wasikivu mnapoagizwa kufanya jambo ili kuepusha vurugu,” alisema Kamanda Kenyela.

No comments:

Post a Comment