19 November 2012

Maalim Seif aupongeza uongozi CCM


Na Mwajuma Juma, Zanzibar

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameupongeza uongozi mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuutaka ufanye kazi zake kwa
kuzingatia misingi ya misingi ya haki na sheria.


Amesema ni wajibu wa viongozi hao kuheshimu sheria za nchi wanapotekeleza majukumu yao na kuepuka kutumia nafasi walizonazo kubariki mambo yaliyo nje ya utaratibu kisheria.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliyasema hayo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Magirisi Melinne, Jimbo la Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi Unguja.

Alisema CUF inaamini kuwa, uongozi huo hautaruhusu kuwepo vikundi visivyokubalika kisheria vinavyodaiwa kuhusika na vurugu pamoja na kunyanyasa wananchi.

Aliongeza kuwa ni vyema viongozi hao wakajipanga zaidi kisiasa
ili Tanzania iweze kuwa na siasa za kistaarabu ambazo zitazingatia ushindani wa hoja na sera.

Maalim Seif aliongeza kuwa, alisema kazi ya vyama vya upinzani katika nchi ni kuikosoa Serikali ili ijirekebishe hivyo hawapaswi kukaa kimya wanapoona kasoro za ukiukwaji wa haki za raia.

“CUF inaendeshwa na dira ya kuitakia mema Zanzibar, hatuwezi kukaaa kimya tunapoona haki za raia zinaingiliwa,” alisema na kuwaomba Wazanzibari kuungana ili kuwa na sauti moja wanapotetea masilahi ya nchi yao.

Akizungumzia mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya, aliwataka wannchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kujiandaa na
kutoa maoni yao kuanzia Novemba 19 mwezi huu.

Aliiomba tume inayoratibu mchakato wa kukusanya maoni hayo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Joseph Warioba, kuweka utaratibu mzuri ambao utawawezesha wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa.

Kwa upande wake, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Bw. Hamad Massoud Hamad, alisema chama hicho kina mpango
wa kufanya uhakiki mpya wa wanachama wake ili kuimarisha
uhai wa chama katika maeneo yote nchini.

Katika mkutano huo, Maalim Seif alikabidhi kadi kwa wanachama wapya 92 ambao waliamua kujiunga na chama hicho.

No comments:

Post a Comment