19 November 2012

Bilal kuongoza muadhara wa kumuenzi Moringe Sokoine



Na Aziz Msuya, Morogoro

MAKAMU wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, anarajiwa
kuwa Msemaji Mkuu katika muadhara utakaofanyika leo katika Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro, Kampasi ya Solomon Mahlangu ili kuadhimisha kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Moringe Sokoine.


Akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo jana, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Gerald Monela, alisema muadhara huo utakuwa wa wazi wenye mada inayosema “Mageuzi ya Kisiasa na Demokrasia Huria Tanzania, Urithi aliyotuachia Edward Moringe Sokoine”.

“Huu ni mwaka wa 13 kufanya maadhimisho haya na mwaka huu utaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili, ili kumuenzi Hayati Sokoine kwa kutambua mchango wake na kuwapa fursa wanazuoni kujadili kiazi zake, mitazamo na matendo yaliyotukuka.

“Tunamuenzi Hayati Sokoine ili asisahaulike, mazuri yake yaendelee kutumika na kutukuzwa kama uadilifu wake, kazi
zake, uwajibikaji na kukemea rushwa,” alisema Prof. Monela.

Aliongeza kuwa muhadhara wa kwanza wa kumbukumbu ya kumuenzi Sokoine ulifanyika Aprili 14,1992 na uliongozwa
na Hayati Rashid Mfaume Kawawa aliyewahi kuwa Makamu
Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais.

“Katika madhara hii, kulikuwa na mada mbalimbali kila mwaka kutokana na fikra pamoja na falsafa Hayati Sokoine zinavyoweza kuakisi mageuzi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wakati huu ambao tuko nao,” alisema.

Prof. Monela ametoa wito kwa wanazuoni na wananchi wote wa ndani na nje ya Morogoro, kuhudhuria muhadhara huo ambao utaanza asubuhi na kutatoa fursa kwa watu kutoa michango yao.

“Chuo hiki kinatumia jina la kiongozi huyu ambaye amekua Waziri Mkuu kwa vipindi viwili 1977-1980 na 1983-1984, hivyo tunalo jukumu kubwa la kumuenzi kwa kutafakari mambo mbalimbali aliyolifanyia Taifa hili,” alisema Prof. Monela.

No comments:

Post a Comment