19 November 2012

Ponda, wenzake waikana BAKWATA



Na Rehema Mohamed

WASHTAKIWA 49 akiwemo Shekhe Ponda Issa Ponda ambao wanakabiliwa na kesi ya kuvamia kwa nguvu ardhi ya Kampuni
ya Agritanza Ltd, wamelikana Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA) kuwa haikusajiliwa kwa ajili ya Waislamu wote.

Shekhe Ponda na wenzake, waliikana BAKWATA katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana
baada ya kusomewa maelezo ya awali na wakili wa Serikali
Bw. Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Victoria Nongwa, anayesikiliza kesi hiyo.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, wakili wa utetezi Bw. Nassor Juma, aliieleza Mahakama hiyo mambo yanayobishaniwa katika
hati ya maelezo ya awali moja wapo ni washtakiwa hao kuikana BAKWATA kuwa haikusajiliwa kwa ajili ya Waislamu wote.

Hata hivyo, alibainishwa kuwa pamoja na washtakiwa kulikana baraza hilo, bado wamekubali uwepo wake pia wamekubali
kukamatwa na polisi Oktoba 16 mwaka huu na kufikishwa Mahakamani Oktoba 18 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, wakili huyo aliulalamikia upande wa mashtaka kwa kumpeleka Shekhe Ponda katika chumba cha
Mahakama akiwa amefungwa pingu mikononi.

Alisema upande wa mashtaka unatakiwa uheshimu haki za binadamu hivyo wanapaswa kuondoa utaratibu huo na kama wanapenda kumfunga pingu mshtakiwa, wafanye hivyo
akiwa nje ya mahakama ambapo ombi hilo lilikubaliwa na
Hakimu Nongwa ambaye alilitilia mkazo.

Wakili Juma pia aliomba kupatiwa maelezo ya mlalamikaji
katika shauri hilo, kupewa idadi ya mashahidi na vielelezo
ambayo vitatumika wakati kesi hiyo inasikilizwa na
kuahidiwa kupewa.

Kabla washtakiwa hao hawajasomewa maelezo ya awali, upande wa mashtaka uliwasomea upya washtakiwa wote mashtaka yao baada ya hati hiyo kufanyiwa mabadiliko.

Mabadiliko hayo ni pamoja na kuongezwa mshtakiwa mwingine Sheikh Mukadamu Salehe na kuondolewa kwa mshtakiwa Rashid Juma ambaye alifutiwa mashtaka na Mkurunenzi wa Mashtaka
nchini  (DPP)

Akiwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao, Bw. Kweka alidai BAKWATA ni taasisi iliyoundwa ili kutoa miongozi na uwakilishi wa Jumuiya za Kiislamu nchini.

Alidai baraza hilo lipo chini ya wadhamini wake na linamiliki mali mbalimbali ikiwemo ardhi iliyopo eneo la Chang'ombe Markas.

Juni 18 mwaka huu, BAKWATA kupitia wadhamini wake waliingia katika makubaliano ya kuuza eneo hilo kwa Kampuni ya Agritanza Ltd ambapo makubaliano hayo yaliambatana na malipo ya fedha pamoja na kupewa eneo lingine lililoko Kisarawe.

Makubaliano hayo yaliifanya ardhi hiyo ya kubalishwa umiliki ambapo Oktoba 12 mwaka huu, ambapo baada ya kampuni hiyo kuanza ujenzi washtakiwa hao kwa pamoja ambao ni wafuasi wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini walivamia eneo hilo wakiongozwa na Shekhe Ponda na Shekhe Mukadamu.

Ilidaiwa kuwa, wafuasi hao baada ya kuvamia eneo hilo kijinai walikaa hadi Oktoba 16 mwaka huu, ambapo wakiwa eneo hilo waliharibu malighafi za ujenzi na msingi uliokuwa umeanza kujengwa na kampuni hiyo.

Oktoba 16 mwaka huu, washtakiwa hao walikamatwa na polisi ambapo Oktoba 18 mwaka huu, walifikishwa mahakamani hapo
na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 29 mwaka huu itakapoletwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Katika kesi hiyo washtakiwa hao wanadaiwa Oktoba 12 mwaka huu, huko eneo la Chang'ombe Markas, walikula njama ya kutenda makosa hayo.

Shtaka la pili, washitakiwa hao wanadaiwa Oktoba 12 mwaka huu,  huko Chang'ombe  Markas, kwa jinai wasipokuwa na sababu za msingi washitakiwa hao waliingia  katika kiwanja ambacho kinamilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd, kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu, huko Chang'ambe Markasi, pasipo na uhalali wowote, walijimilikisha kwa nguvu ardhi ya kampuni hiyo.

Shitaka la nne ilidaiwa Oktoba 12-16 waka huu, washitakiwa hao waliiba vifaa, malighafi, matofali 1,500, nondo, tani 36 za kokoto vyote vikiwa na thamani ya sh. 59,650,000 mali ya kampuni  hiyo.

Katika shtaka la tano ni uchochezi linalomkabili Shekhe Ponda na Shekhe Mukadamu ambapo ilidaiwa Oktoba 12-16 mwaka huu, katika eneo la Chang'ombe Markas, waliwashawishi wafuasi wao (washtakiwa), kutenda makosa hayo.

No comments:

Post a Comment