19 November 2012

TAKUKURU yawaburuta kortini wasimamizi mradi wa mfereji


Na Mashaka Mhando, Tanga

VIONGOZI waliokuwa wakisimamia Mradi wa Ujenzi wa Mfereji wa Maji ya Mvua, Mtaa wa Azimio jijini Tanga na Mhandisi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoani humo, wamefikishwa katika Mahakamani ya Wilaya ya Tanga, wakikabiliwa na kesi ya kutumia vibaya madaraka yao.

Shtaka jingine linalowakabili washtakiwa hao ni kula njama
ili kumnufaisha fundi aliyejenga mtaro huo kujipatia fedha
kinyume cha taratibu.

Kesi hiyo imefunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambapo mshtakiwa wa kwanza ni Bw. Julius Kahangi, ambaye ni Mtaalamu Mshauri wa mradi kutoka halmashauri ya jiji hilo na Mhandisi Bona Mtui (Mkaguzi wa
nje wa mradi huo kutoka TANROADS).

Wengine ni Mwenyekiti wa mradi huo, Bi. Mariam Haji, Bw. Mpemba Mwakuluzo (Katibu wa Kamati ya Mradi), Bw. Salimu Amir (Mweka Hazina), na fundi aliyejenga mtaro huo Bw.
Lawrent Senyenge.

Akiwasomea mashitaka hayo, Mwanasheria wa TAKUKURU, Bw.  Samuel Gabriel, alisema mshitakiwa wa kwanza na wa pili (Kihengi na Mtui), wanatuhumiwa kutumia madaraka yao vibaya chini ya kifungu cha 31 cha taasisi hiyo na Bw. Senyenge, kujipatia fedha kutoka TASAF, huku wakijua kazi aliyopewa haikukamilika kwa mujibu wa taratibu.

Washtakiwa wengine (Mariamu, Salimu, Mwakuluzo na Senyenge) wanadaiwa kula njama ya kula rushwa na kutoa tenda bila kupitia taarifa za manunuzi badala yake walikaa kikao hewa na kupitisha jina la Bw. Senyenge kinyume cha taratibu.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Bw. Maira Kasondi, Mchunguzi wa TAKUKURU mkoani humo, Bw. Edwin Samuel, alisema TASAF ilitoa fedha sh. milioni 19,
kwa ajili ya mradi ulioibuliwa na wananchi wa mtaa huo huo
wa kuchimbiwa mtaro wa maji wenye urefu wa mita 1,440.

“Kwa kuzingatia utaratibu, utaratibu TASAF inatoa fedha asilimia 80 na iliyobaki, inapaswa kutolewa na wananchi lakini katika mradi huu, wananchi hawakutoa, mfereji ulijengwa kwa fedha za mfuko.

“Baada ya kukamilika, TASAF wakaomba mtaalamu (Mhandisi Mtui wa TANROADS), ambaye ni mshtakiwa wa pili, alipoukagua mtaro huu pamoja na mshtakiwa wa kwanza, alindika taarifa na kudai mtaro umekamilika kwa asilimia 100, ukiwa na urefu wa
mita 889 na wananchi wametoa fedha jambo ambalo ni uongo,” alisema Bw. Samuel.

Alidai kuwa, baada ya taarifa hiyo, TASAF walitoa cheti kwa fundi aliyejenga mtaro huo na kulipwa fedha zote zilizotengwa lakini baadaye baadhi ya wananchi walilalamikia mtaro huo kujengwa chini ya kiwango licha ya taarifa ya Mhandisi Mtui kudai kuwa, umejengwa kwa kufuata tartibu zote.

“Baada ya kupokea malalamiko ya wananchi, tuliunda timu ya kwenda kuchunguza nikiwemo mimi (Samuel), Mwenyekiti wa Mtaa Bw. Mohamed Kassim, Mratibu wa TASAF jijini humo, Bw. Ramadhani Possi, Mhandisi wa jiji hilo, Bw. Julius Kihengi na Mhandisi wa TAKUKURU Makao Makuu, Christopher Shewele na baada ya kuupima mtaro, ulikuwa na urefu wa mita 754.1,” alisema.

Aliongeza kuwa, fedha zilizotolewa za TASAF, asilimia 80 zilipaswa kutumika kujenga mtaro huo kwa sababu wananchi hawakutoa nguvu zao hivyo ungekamilika kwa mita 1,154, lakini
umejengwa kwa mita 754.1, sawa na asilimia 50 hivyo wote walioshiriki walifanya njama za kula rushwa.

Akiwazungumzia wasimamizi wa mradi huo, Bw. Samuel alisema kamati ya ujenzi haikufuata utaratibu wa kumtafuta mzabuni wa kujenga mtaro huo badala yake walikaa kikao chao bila kuwa na nukuu za wazabuni hivyo kuleta mashaka kuwa huenda tenda hiyo alitolewa kinyume cha sheria.

Hata hivyo, wakili wa mshtakiwa wa kwanza na wa pili Bw. Mwita Kichere, aliitaka TAKUKURU waifungulie mashtaka TANROADS badala ya mteja wake Mhandisi Mtui, kwani barua zilizotolewa kama ushahidi wa kuomba mtaalamu, hazikutoa maelekezo ya
jina na kutaka TASAF ishtakiwa kwa kutoa fedha hizo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 17 mwaka huu ambapo washtakiwa wengine watano watatoa ushahidi wao Januari 15 mwakani. Washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment