29 November 2012
Kili Stars yakwaa kisiki Namboole
Na Mwandishi Wetu, Kampala
TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), jana ilikwaa kisiki baada ya kufungwa bao 1-0 na Burundi katika mechi ya michuano ya Chalenji iliyochezwa Uwanja wa Mandela.
Kilimanjaro Stars sasa italazimika kushinda mechi yake dhidi ya Somalia, ili iweze kuweka matumaini yake hai ya kutinga robo fainali.
Mechi hiyo ilianza kwa kasi licha ya uwanja kujaa tope kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kabla ya kuanza, ambapo Kilimanjaro Stars ilikosa bao dakika ya 27 kupitia kwa Saimon Msuva na Mrisho Ngassa alikosa dakika ya 29 lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.
Baada ya mashambulizi hayo, Burundi walijipanga na kuanza kupeleka mashambulizi langoni mwa Kili Stars,ambapo dakika ya 39 ambapo mshambuliaji wake Steve Nzigamasabo alikosa bao la wazi.
Safu ya ushambuliaji wa Burundi iliongozwe na mshambuliaji wake mkongwe Suleiman Ndikumana, hata hivyo hakuweza kupenya ukuta wa Kili Stars, uliokuwa chini ya Kelvin Yondan na Shomari Kapombe.
Katika kipindi hicho kocha wa Kili Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen alimtoa, Msumva na kumwingiza Amri Kiemba ambaye aliiongezea nguvu timu hiyo.
Dakika ya 41 Kiemba nusura aipatie Kili Stars bao lakini shuti lake likapanguliwa na kipa wa Burundi.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mashambulizi langoni mwa mpinzani wake.
Dakika ya 51 Burundi ilipata bao kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Ndikumana ambaye awali alifanyiwa madhambi na Kapombe katika eneo la hatari, hivyo mwamuzi Ronnie Kalema akaamru penalti ipigwe.
Hata hivyo baada ya Kapombe kucheza madhambi hayo alijigonga vibaya kwa Ndikumana na kulazimika kutoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Issa Rashid 'Baba Ubaya'.
Baada ya bao hilo, Kili Stars ilifanya shambulizi kali langoni mwa Burundi ambapo dakika ya 55, Ngassa aliachia shuti kali lililombabatiza kipa na kuokolewa na mabekSteve Nzigamasaboi.
Dakika ya 62 Ngassa alipata nafasi nyingine nzuri, lakini shuti lake likatoka nje kidogo ya lango la Burundi.
Kili Stars ilifanya shambulizi kali dakika ya 82 ambapo John Bocco 'Adebayor' alipiga mpira kichwa uliookolewa ndani ya mstari, lakini mwamuzi akaamuru ipigwe kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika za mwisho timu zote zilikosa mabao ya wazi, huku mpira wa kichwa uliopigwa na Bocco dakika ya 89 ukigonga mwamba na kurudi uwanjani.
Katika mechi ya kwanza Somalia wameyaaga mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Sudan.Bao la Sudan lilifungwa na Sudan ni Farid Mohammed dakika ya 84.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment