29 November 2012

Serikali yatoa kauli nzito *Simanzi vilio vyatawala msibani




Na Benedict Kaguo,Muheza

SERIKALI wilayani Muheza imetoa muda wa saa 24 vinginevyo italazimika kutumia nguvu ya dola kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wananchi wote wa Kijiji cha Songa Kibao Maguzoni waliohusika na wizi
wa mali za Msanii Hussein Ramadhan Mkieti 'Sharo Milionea', aliyezikwa jana Lusanga Muheza.


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muheza ,Subira Mgalu,  wakati akitoa tamko la Serikali kutokana na aibu hiyo iliyojitokeza wakati wa tukio la ajali ambapo msanii huyo aliibiwa mali zote ikiwa ni pamoja na nguo alizovaa.

Alisema Serikali itatumia nguvu kuwasaka watu hao kwa sababu inajulikana waliohusika na wizi huo na kutahadharisha kuwa wajisalimishe wenyewe kabla hatua ya kuvamia kijiji hicho
na kutumia nguvu ya dola haijafanyika.

Mgalu alitoa saa 24 kuhakikisha vitu vyote vilivyoibwa vinasalimishwa na baada ya hapo nguvu itatumika kuwasaka
watu wote na watakamatwa na kufikishwa Mahakamani.


Hali wakati wa mazishi


Vilio na simanzi viligubika jana katika Kijiji cha Lusanga wilayani Muheza wakati wa Mazishi ya msanii huyo maarufu wa sanaa ya maigizo maarufu kama Sharo Milionea, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nauye akiongoza mamia ya waombolezaji.

Hali ya simanzi ilitikisa hasa wakati ambapo mwili wa marehemu ulikuwa ukiwasili kijiji hapo kutokea Hospitali Teule ya Muheza, ambapo mwili wake ulihifadhiwa baada ya kutokea ajali iliyosababisha kifo.

Mazishi hayo ambayo yalihudhuriwa na wasanii mbalimbali wa Bongo Movie, ambapo Nape alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye mazishi hayo.

Akizungumza wakati wa mazishi hayo Nape alisema Serikali ya CCM imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo hicho kwani amefariki dunia akiwa na umri mdogo, tena akiwa ndiyo anaanza kufanikiwa kimaisha .

Alisema umati uliojitokeza kwenye mazishi hayo ni ishara ya msanii huyo kukubalika na jamii na kutaka iwe fundisho kwa wasanii wengine kujituma kwani Taifa linatambua mchango wao.

Alisema kifo cha msanii huyo ni funzo kwa wasanii kuyaenzi yote aliyofanya enzi za uhai wake na kwamba umati wa watu waliojitokeza kumzika ni ishara tosha ya kukubalika ndani ya jamii.


Alisema upendo na mshikamano uliooneshwa na wasanii wa Bongo Movies ni ishara ya kukua kwa tasnia hiyo na kueleza kuwa Serikali itaendelea kupigania haki za wasanii na kwamba mchango wake utaendelea kuenziwa katika tasnia hiyo.

Alisema haki zake marehemu zipatikane na zipewe familia yake na kutaka jukumu hilo kuendelea kutekelezwa ili kuendelea kukuza fani hiyo ya filamu.


Matukio yaliyojiri

Waombolezaji mbalimbali wakiwemo ndugu wa marehemu walizimia kwa saa kadhaa na kukimbizwa Hospitali Teule ya Muheza ambapo walilazwa na kupatiwa matibabu.

Dada wa marehemu, Halima Mkiheti ambaye ni mjamzito alizimia kwa nyakati tofauti.

JB,RAY wafunika msibani


Msanii Jacob Steven JB alijikuta akishangiliwa na waombolezaji waliofika msibani huku watu wakitoka kwenye majonzi na kujikuta wakipiga kelele za kumshangilia na kumkumbatia hadi alipoondolewa na walinzi hadi kwenye gari aina ya Coaster walilokuwa wamekwenda
nalo msibani.

Mwingine aliyetikisa msiba huo ni Vicent Kigosi ‘Ray’ pamoja na Diamond ambao muda mwingi walikuwa wakishangiliwa na waombolezaji hadi walipoondoka eneo hilo la msiba.

Rais Kikwete amlilia

Rais Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha msaani huyo, ambapo alisema ni pigo kubwa kwa tasnia hiyo. Pia salamu zake alizielekeza kwa familia ya marehemu na jamaa wengine walioguswa na msiba huo.

No comments:

Post a Comment