26 November 2012

JK apokea taarifa ya maendeleo ujenzi wa kampasi tiba za afya


Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete, jana amepokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa kampasi mbili za tiba ya afya zinavyojengwa katika
Chuo Kikuu cha Dodoma na Mloganzila huko Kisarawe,
ambazo pia zitatumika kama hospitali.

Awali Rais Kikwete alipokea maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Afya Chuo Kikuu cha Dodoma kutoka kwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (NHIF), Bw. Emmanuel Humba.

Ujenzi wa kampasi hiyo umeshaanza na kufikia hatua nzuri ambapo hospitali inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2015.

Bw. Humba alisema, maandalizi ya kufanikisha uanzishaji wa
Chuo na hospitali hiyo yameanza ambapo baadhi ya wataalamu wakiwemo madaktari na watumishi wengine wako nchini na nje
ya nchi kwa ajili ya masomo na mafunzo mbalimbali.

Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya kisasa vya tiba ambavyo vitakidhi mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari kwa kiwango cha kimataifa.

Rais Kikwete pia alipokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila ambapo katika ujenzi na uanzishwaji wa Kampasi hizi zote, amesimamia kuanzia hatua za awali.

Kampasi ya Mloganzila ambayo ni sehemu ya Hospitali Kuu ya Muhimbili inajengwa kwenye eneo la ekari 3,800 na itakua sehemu ya kutolea mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na huduma za afya pia ni sehemu ya kutolea matibabu ya maradhi makuu na kawaida.

Ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa Januari 2013 na unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada ya ujenzi.

Katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Profesa Ephata Kaaya, alitumia fursa hiyo   kumkabidhi Rais Kikwete, Cheti cha Udaktari wa Public Health (Honoris Causa), kutokana na Shahada aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili Desemba 2010 kwa kutambua mchango wake wa kuendeleza sekta ya afya nchini.

Akitoa taarifa ya maendeleo kwa Rais Kikwete, Prof. Kaaya alisema tayari wataalamu na wafanyakazi wanaotarajiwa kufanya kazi katika kampasi ya Mloganzila wameanza mafunzo.

Alisema ujenzi wa hospitali hiyo ukikamilika, itakua na
vitanda vya kulaza wagonjwa 600 ambapo Rais Kikwete
aliwapongeza wataalamu wote kwa juhudi zao na kusema
kuwa, lengo lake ni kuhakikisha nchi inaondokana na adha
ya kupeleka wagonjwa nje kwa ajili ya matibabu.

1 comment:

  1. katika hili nakupongeza mheshimiwa Raisi kikwete na serikali yako kwa ujumla......

    ReplyDelete