26 November 2012

Urais 2015 CHADEMA moto *Zitto aanika msimamo wake, atoa neno


Na Rehema Maigala

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema kama chama chake hakitampa ridhaa ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, ataachana na ubunge.

Bw. Kabwe aliyasema hayo juzi katika mahojiano maalumu na Mtandao wa Jamii Forums na kusisitiza kuwa, mbali ya kuachia ubunge atakuwa tayari kumpigia debe mgombea urais ili chama
hicho kiweze kushika dola katika uchaguzi huo.

Alisema mwaka 2010, mgombea urais wa chama hicho Dkt. Willibrod Slaa alikuwa peke yake bila msaidizi wa kumpigia
debe hivyo uamuzi wake utakuwa sahihi.

“Tayari nilishawaeleza wakazi wa Kigoma kuwa nitakaa katika kiti cha ubunge kwa vipindi viwili tu, baada ya hapo nitagombea urais ambao upo ndani ya damu yangu ndio maana nataka chama changu kinipe ridhaa ya kugombea mwaaka 2015,” alisema Bw. Kabwe.

Aliongeza kuwa, kama chama hicho hakitampa ridhaa hiyo, bado ana ndoto ya kuwa Waziri aweze kutekeleza mabadiliko ambayo Watanzania wanayasubiri katika harakati za chama hicho kusaka ukombozi wa kweli.

Bw. Kabwe alipoulizwa kuhusu chama chake kuwa cha kidini
na ukabila alidai kuwa, madai hayo hayana ukweli wowote bali CHADEMA ni cha Watanzania wote.

Alisema baadhi ya wanachama wa chama hicho ni mabingwa wa kueneza jambo na kupandikiza mbegu za chuki ili Chama Cha Mapinduzi (CCM), kipate nafuu ya kuzungumza.

Akizungumzia kauli ya Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa, juu ya ushauri wake kwa Serikali kutoa elimu ya bure kwa shule za sekondari Bw. Kabwe alisema;

“Naomba nilizungumzie hili, mwaka 2010 CHADEMA kupitia sera yetu tulisema, kama tutapata ridhaa ya kuongoza nchi, tutatoa elimu ya sekondari bure lakini tukaitwa wendawazimu.

“Tuliulizwa tutawezaje kusomesha idadi kubwa ya wanafunzi wakati hatuna msingi wowote wa maendeleo, hivi sasa kauli hii imejirudia, ninachoona mimi viongozi wetu ni wazembe kwani hawazingatii kauli wanazotoa, wameonesha udhaifu mkubwa,” alisema.

Akizungumzia Katiba, Bw. Kabwe alisema mfumo mzima wa
katiba unapaswa kubadilishwa kwani yote ina kasoro mbalimbali ambapo katiba makini ni ile inayowapa matumaini Watanzania badala ya kuwakandamiza kama ilivyo sasa.

Makala kamili ya mahojiano kati ya Bw. Kabwe na mtandao huo itatoka Jumapili katika gazeti hili usikose kuisoma.

No comments:

Post a Comment