28 November 2012

DC awabana vigogo wa serikali *Aagiza wanyang'anywe ardhi waliyopewa


Na Yusuph Mussa, Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, ameagiza vigogo wote wa Serikali waliopewa ardhi kinyembela kwenye Kata ya Mswaha-Darajani, Tarafa ya
Mombo, wanyang’anywe akiwemo Bw. Jonas Malorsa
(aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri Wilaya ya
Korogwe), ambaye hivi sasa amesimamishwa kazi.

Bw. Gambo alitoa agizo hilo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Mswaha, baada ya kutembelea
Hifadhi za Msitu wa Mswaha na kuitisha kikao na wananchi.

“Baada ya maelezo ya wananchi, nimebaini watu wengi waliopewa ardhi wametumia njia ya ujanja ujanja kwa viongozi wa vijiji lakini sio ridhaa ya wananchi hivyo wanyang’anywe na ibaki huru hadi  itakapofanyiwa tathmini.

“Pia nataka wahamiaji wote haramu wanaokaa kinyume cha utaratibu, waondoke na kurudi walikotoka la sivyo wafuate
utaratibu, kama watakataa tuelezeni tuwape nguvu ya polisi,”
alisema Bw. Gambo.

Aliongeza kuwa, wahamiaji hao hawakuingia wenyewe bali waliongozwa na viongozi wa vijiji ambao nao wanapaswa
kuchukuliwa hatua za kisheria.

Katika mkutano huo, mkazi wa kijiji hicho Bw. Mohamed Cholido, alimtaja Bw. Malorsa kuwa ni miongoni mwa watu waliotumia cheo chake kuwarubuni wanakijiji, kwani alitoa sh. 500,000 kwa Halmashauri ya Kijiji hicho kimjadili na kupewa eneo
la ekari 100.

Bw. Cholido alitoa nakala ya mihutasari ya kughushi ambayo inaonesha Bw. Malorsa, alipata baraka ya Halmashauri ya Kijiji pamoja na Mkutano Mkuu wa Kijiji wakati si kweli na kuhoji sh. 500,000 alitoa za nini kwa wajumbe 25.

“Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji walipewa sh. 500,000 na
Bw. Malorsa, pesa hizi za nini wakati hicho si kiwango cha posho tunacholipana tunapokaa vikao, hata hizo ekari 100 hakupewa
na wananchi bali viongozi wa kijiji,” alisema Bw. Cholido.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Bw. Cholido alimkabidhi Mkuu
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Korogwe, Bw. Mussa Chaulo, mihutasari inayoonesha viongozi wa kijiji walighushi ili kuhalalisha Bw. Malorsa kupewa ardhi hiyo.

Hata hivyo, baada ya tuhuma hizo na nyingine kutokana na uuzwaji wa ardhi, wananchi walimtimua madarakani Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw. Juma Mkaka.

Bw. Malorsa alitafutwa kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia madai hayo na kukiri kupewa eneo la kulima lakini sio ekari 100 bali 50, lakini viongozi hao wa kijiji walimuingiza mjini kwani eneo walilompa halipo katika Wilaya ya Korogwe bali Handeni.

“Niliomba eneo na kupewa ekari 50 sio 100 kama wanavyodai lakini wameniuzia eneo la watu wa Handeni, nilipokwenda huko nikakuta viongozi wa kijiji (Kweingoma) wamewauzia wageni kutoka Arusha, hivyo eneo lina mgogoro mkubwa…nimetoa pesa
lakini si kiasi hicho kilichotajwa,” alisema Bw. Malorsa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini Bw. Malorsa alisimamishwa kazi na Mkurugenzi wake, Mhandisi Anna Mwahandele, kupisha uchunguzi wa matumizi mabaya
ya fedha katika idara yake.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mwahandele, naye amesimamishwa kazi mwezi mmoja uliopita ili aweze
kuendelea na kesi inayomkabili mjini Moshi.

1 comment:

  1. DED kamwaga ugali wa DT na DT kawezesha mboga ya DED kumwaga na ana kesi nani yuko nafuu anachunguzwa huku akila mshahara wote au yule aliye na kesi na kula nusu mshahara.akili ku mkichwa

    ReplyDelete