28 November 2012

Vigogo wa TAZARA wapewa dhamanaNa Rehema Mohamed

MHANDISI Mkuu na Meneja wa Fedha wa Mamlaka ya Reli
ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ambao juzi walifikishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na tuhuma za kutumia madaraka vibaya
na kuisababishia Serikali hasara ya sh. milioni 120, jana
wamepewa dhamana baada ya kutimiza masharti.


Washtakiwa hao ni Bw. Wenceslaus Kamugisha (Mhandisi),
na Bi. Sarah Masiliso (Meneja wa Fedha), ambao walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu
Frank Mosha.

Masharti waliyosomewa jana ni kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali au taasisi inayotambulika.

Wadhamini walitakiwa kusaini dhamana ya sh. milioni 10, ambapo mdhamini au mshitakiwa alipaswa kuwasilisha fedha taslimu sh. milioni 30 au mali isiyohamishika inayofikia thamani hiyo na washitakiwa wote kutoruhusiwa kutoka nje ya Dar es Salaam
bila kibali cha Mahakama.

Washtakiwa hao walidhaminiwa kwa hati moja ya nyumba yenye thamani ya sh. milioni 62, iliyotolewa na wadhamini wao.

Katika kesi hiyo, ilidaiwa Aprili mwaka huu, washtakiwa hao wakiwa wafanyakazi wa TAZARA, walitumia madaraka vibaya
kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao na kuongeza maombi katika mchakato wa zabuni kwa nia ya kupata faida kutoka
Kiwanda cha Chrinikap.

Wakili wa Serikali ambaye aliwasomea mashtaka hayo, Bw. Tumaini Kweka, alidai washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kati ya Aprili mwaka huu, waliisababishia Serikali hasara ya sh. milioni 120.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 10 mwaka huu, itakapoletwa kwa ajili ya kutajwa.

No comments:

Post a Comment